Na Jovina Bujulu- MAELEZO
Wakulima wametakiwa kutumia vizuri
dhamana waliyopewa ya mfumo wa vocha ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya
chakula na biashara kwa maslahi yao na Taifa kwa ujumla.
Wito huo umetolewa jijini
Dar-Es-Salaam na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, Wizara ya Kilimo,
Chakula na Viwanda Richard Kasuga alipokuwa akitoa taarifa ya ruzuku ya
pembejeo za kilimo kwa njia ya vocha nchini.
Kasuga aliendelea kusema kuwa
matumizi sahihi ya mbegu bora na mbolea kwa mfumo wa vocha kunaongeza
uwezo wa Taifa kujitosheleza kwa chakula ili kuondokana na umaskini na
kufanikisha mapinduzi ya kijani.
“Vocha ni haki ya mkulima na siyo
upendeleo kwa mkulima anayepatiwa pembejeo hizo, hivyo itumike ipasavyo
ili kuongeza uzalishaji wa mazao husika na kuleta tija katika mazao ya
mahindi na mpunga” alisema ndugu Kasuga.
Katika utaratibu huo wa vocha,
wakulima wa mahindi na mpunga hunufaika kwa kupatiwa pembejeo, ambazo ni
mbegu bora na mbolea zinazotosheleza ekari moja ambapo Serikali
inachangia asilimia 50 ya bei ya soko kwa kila aina ya pembejeo
wanayopewa wakulima hao.
Vigezo vinavyotumika kutoa ruzuku
kwa wakulima nchini ni pamoja na mnufaika kuwa na makazi ya kudumu
katika kijiji na awea analima mpunga au mahindi na kaya iwe tayari
kusaini hati ya pembejeo ili itumie kanuni ya kilimo bora.
Kigezo kingine ni kaya kuwa na eneo
lisilopungua ekari moja pamoja na kaya zinazoongozwa na makundi maalum
hususani wajane na walemavu ndiyo hupewa kipaumbele.
Akizungumzia faida za mfumo huo wa
vocha, ndugu Kasuga alisema kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa uzalishaji
wa chakula, ambapo ongezeko hilo limewezesha wakulima kuuza chakula
ndani na nje ya nchi hivyo kuinua hali zao kiuchumi.
Aidha, Taifa limeondokana na tatizo
la kuagiza chakula nje ya nchi jambo ambalo limesaidia kuokoa fedha za
kigeni hali inayotokana na elimu bora iliyotolewa kwa wakulima ambao
wamehamasika kutumia mbegu bora na mbolea kwa maendeleo endelevu ya
kilimo.
Utaratibu wa kutoa ruzuku ya
pembejeo kutoka Serikalini kwa mfumo wa vocha ulianzishwa na mwaka
2008/2009 ili kuboreka mfumo wa namna ya kuwafikishia wakulima ruzuku ya
mbegu bora na mbolea ambazo hazikuwa zikiwafikia wakulima walengwa
watarajiwa kwa namna iliyotarajiwa.
Ili kuendeleza kilimo chenye tija,
makampuni 23 ya mbolea na 27 ya mbegu bora ya mahindi na mpunga
yanaendelea kutoa huduma ya kusambaza pembejeo hizo katika mikoa
inayolima mazao hayo.
Katika msimu wa kilimo wa 2015/16
mbolea tani 99,993, mbegu bora za mahindi tani 10,271 na tani 815 za
mpunga zitatolewa kuwanufaisha wakulima wapatao 999,926 nchini.
Post a Comment