Aliyegombea
ubunge kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Singida
Mashariki, Jonathan Njau, amepinga ushindi wa Tundu Lissu (Chadema),
akimtaka Msimamizi wa jimbo hilo, Mohammed Nkya, kuruhusu upya uhesabuji
wa kura ili kuondoa utata wa kisheria.
Akizungumza
na waandishi wa habari mjini hapa mwishoni mwa wiki, Njau alisema iwapo
msimamizi huyo atashindwa kutekeleza ombi hilo, hatakuwa na njia
nyingine zaidi ya kwenda mahakamani kuhoji matokeo hayo.
Katika
uchaguzi huo, Lissu alitangazwa mshindi, baada ya kujizolea kura
24,874, akifuatiwa na Njau kwa kura 18,393, huku Vedatus Muna, wa
ACT-Wazalendo akipata kura 241 na Msafiri Sprian, wa Chama cha Wananchi
(CUF), akiambulia kura 85.
Njau
alisema kuwa ili haki ipatikane, anaomba uhesabuji kura ufanywe upya
kwa madai kwamba Msimamizi wa Uchaguzi alikiuka kanuni na baadhi ya
vifungu vya sheria za uchaguzi.
Alidai
kuwa kanuni inamtaka msimamizi wakati wa kuhesabu kura kuhakikisha
masanduku yote yamepokelewa, lakini hakufanya hivyo, hali inayotia shaka
kwa matokeo aliyotangaza.
Alilalamikia
pia ujumulishaji wa kura akidai lazima ufanywe kwa kufuata matokeo ya
kura za kituo kwa sababu kila kituo kilikuwa na sanduku lake.
Post a Comment