Aliyekuwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salvatory Rweyemamu amemaliza mkataba
wake na kuondoka huku akiwashukuru watendaji kwa muda wote aliokuwa nao
wakimsaidia Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Mrisho Kikwete.
Kuondoka
kwake kunampa fursa Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli kuunda safu
mpya ya Kurugenzi ya Mawasiliano. Salva aliteuliwa, kwa mara ya kwanza,
na Rais Kikwete kushika wadhifa huo Septemba 17, 2007 na alimaliza
mkataba wake Septemba 11, 2015 lakini aliongezewa hadi Novemba 10.
Baada
ya Dk Magufuli kuapishwa Novemba 5, Rais Kikwete aliondoka siku
iliyofuata kurudi nyumbani kwao Msoga, Chalinze, na kwa kuwa Salva
amemaliza pia muda wa nyongeza ameondoka na kurudia majukumu yake ya
awali.
Kabla
ya kuteuliwa kusimamia Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu Salva alikuwa
mmoja wa wamiliki na Mhariri Mtendaji wa kampuni ya Habari Corporation
(sasa New Habari Corporation). Mwaka huo, aliteuliwa kuziba nafasi
iliyoachwa wazi na Peter Kallaghe aliyeteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania
nchini Canada.
Akizungumza
na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki iliyopita Salva aliweka wazi
kuwa ataondoka katika ofisi hiyo Jumatatu ya wiki hii (jana) na
kumkaimisha msaidizi wake, Mwandishi wa Rais Msaidizi, Premi Kibanga
kuendelea na majukumu yatakayojitokeza.
“Nimetumika
Ikulu kwa zaidi ya miaka minane na kwa kipindi hicho chote nimesaini
mikataba kadhaa ya kuendelea na kazi. Wakati umefika wa mimi kuondoka.
Nawashukuru viongozi wa Ikulu pamoja na Rais Kikwete aliyeniamini kuwa
msaidizi wake. Nampongeza Dk Magufuli pia kwa kuchaguliwa kwake
kuendelea kuwatumikia Watanzania,” alisema Salva ambaye pia aliwahi kuwa
mkurugenzi wa kampuni ya mawasiliano ya umma ya S & G.
“Mkataba
wangu wa mwisho wa kazi uliisha Septemba 11, 2015 kabla sijaongezewa
mwingine unaokamilika Novemba 10 na siku hiyo nitaikabidhi ofisi kwa
Premi Kibanga. Nimemaliza kuweka mambo yote sawa tangu Jumapili.
Ninaondoka nikiwa mwenye furaha, nilishirikiana vyema na Makatibu Wakuu;
Philemon Luhanjo na Balozi Ombeni Sefue,” alisema.
Aidha,
amewashukuru waandishi wa habari kwa ushirikiano waliompa kwa kipindi
chote alichohudumu kwenye kurugenzi hiyo mpaka wakati huu anapoondoka.
Post a Comment