MWENYEKITI
wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu
amepuuza shinikizo toka kwa baadhi ya wanachama wa chama hicho, Iringa
Mjini, linalomtaka aachie ngazi kwa tuhuma kwamba amechangia chama hicho
kipoteze jimbo na kata 14 kati ya 18 za Iringa Mjini.
Pamoja
na Msambatavangu, wengine wanaotakiwa kuachia ngazi kwasababu ya tuhuma
hiyo ni Mwenyekiti wa UVCCM Iringa Mjini, Kaunda Mwaipyana na
Mwenyekiti wa UVCCM Kata ya Mkwawa, Salum Keita.
Mbali
na viongozi hao, wanachama hao wamemtaka Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina
Masenza kwa mamlaka aliyopewa na Rais wa Jamuhuri wa Muungano wa
Tanzania ahakikishe, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa
ambaye pia ni Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Iringa Mjini anaondolewa
kazini kwa kuwa ameshiriki kuvuruga uchaguzi katika jimbo hilo.
Wakati
Jesca, Kaunda na Keita wanatuhumiwa kutumia nafasi zao kuwashawishi
wapiga kura wa Iringa Mjini kutowachagua wagombea wa CCM katika ngazi ya
udiwani, ubunge na urais, Msimamizi wa Uchaguzi anatuhumiwa kutupilia
mbali ombi la chama hicho na mgombea wake lililotaka kura za ubunge za
jimbo hilo zihesabiwe upya.
Msimamizi
huyo wa uchaguzi ambaye majira ya saa nne usiku ya Jumatatu ya Oktoba
26, alishikiliwa na Polisi kwa muda anatuhumiwa na CCM kufungua baadhi
ya maboksi ya kura zilizokwishapigwa akiwa pamoja na wanachama nane wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema); tuhuma ambazo kaziknusha
kwamba si za kweli.
Tuhuma
nyingine kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa hivikaribuni na Katibu wa
CCM Mkoa wa Iringa, Hassan Mtenga inahusu kuchelewa kupata taarifa ya
marudio ya uchaguzi katika kituo cha Ipogolo C kilichovamiwa na watu
wasiojulikana Oktoba 25 na kuibiwa na maboksi mawili ya kura wakati
zoezi la uhesabuji kura likiendelea.
Mtenga
alisema jambo lingine wanalolilalamikia kujitokeza Oktoba 25 wakati wa
upigaji kura ni lile linalohusu mawakala wake kuzuiwa kutumia simu
wakati kuna ushahidi wa baadhi ya mawakala wa Chadema kuruhusiwa kutumia
mtandao huo wa simu.
Akikanusha
madai ya CCM dhidi yake, Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo hilo alisema;
“ninaifanya kazi yangu kwa weledi mkubwa na kwa kuzingatia sheria za
nchi na sheria zote za uchaguzi.”
Alisema
hakuna wakala aliyeruhusiwa kutumia simu katika kituo cha kupigia kura
kama taratibu zinavyotaka na akazungumzia utaratibu wa kisheria
uliotumika kuwapata wasimamizi wasaidizi ambao alisema hawapatikani kwa
itikadi zao za vyama.
Kuhusu
kukamatwa na Polisi, Sawa alikiri kuitwa na Polisi kwa mahojiano baada
ya kuwepo kwa tetesi zilizomuhusisha yeye na maafisa wengine wa tume na
wanachama wa Chadema kufungua maboksi ya kura na kuzihesabu kura hizo
bila wawakilishi wa vyama vingine kuwepo.
Sawa
alisema madai hayo sio ya kweli na kwamba wakati tukio la kuchukuliwa
na Polisi likitokea walikuwa wakiendelea kutekeleza majukumu yao,
ikiwemo kutuma NEC matokeo ya kura za rais.
Naye
Msambatavangu alisema shinikizo la kikundi cha wanachama wa Iringa
Mjini wanaomtaka ajiuzulu linalotokana na majungu, fitina na vikundi vya
uasi vinavyoanzishwa na baadhi ya viongozi ndani ya chama kwa lengo la
kulinda maslai ya watu fulani.
“Hivi
inawezekaneje mimi na hao wachache tunaotajwa, tukavumiliwa katika
kipindi chote cha kampeni tufanye kazi ya kikihujumu chama mpaka baada
ya kupoteza jimbo na kata ndio tuseme, wakati kazi hiyo ya kukihujumu
chama inafanyika wana CCM na viongozi wengine walikuwa wapi, maana CCM
ina mtandao mpaka ngazi ya balozi” alisema.
Alisema
kuna njama za kumchafua yeye na viongozi wengine ndani ya chama hicho
kwa maslai ya watu fulani kwasababu kuna blanda zilifanyika kinyume na
utaratibu kabla ya mchakato wa kura za maoni.
Msambatavangu
alisema kama angekuwa mtaalamu wa kutumia hujuma zinazodaiwa na
wanachama hao, isingekuwa rahisi kwake kushindwa kura za maoni za
kuwania nafasi hiyo ya ubunge dhidi ya aliyekuwa mgombea wao Frederick
Mwakalebela.
“CCM
Iringa Mjini ina wanachama 26,000; sasa kama nilishindwa kutumia hujuma
waanazosisema kuwashawishi wanachama hao wanipigie kura wakati wa kura
za maoni, ninawezaje kumsaidia kwa hujuma hizo hizo Mchungaji Msigwa
ashinde ubunge jimbo la Iringa Mjini kwa kupata kura zaidi ya 43,000,”
alisema.
Jesca
alihoji kwanini wanachama hao wasishinikize viongozi wa wilaya na kata
walizopoteza ndio waondoke na badala yake wanamnyoshea kidole yeye huku
wakijua yeye ni kiongozi wa mkoa ambaye majimbo yote saba ya uchaguzi
yako chini yake.
Alisema
katika mchakato wa uchaguzi huo ametumia fedha zake, rasilimali zake na
umaarufu wake kukiimarisha chama katika majimbo yote ya mkoa wa Iringa
na katika kampeni za Iringa Mjini alifanya mikutano ya kata kwa kata
sambamba na mgombea ubunge wa jimbo hilo, Mwakalebela.
Akizungumzia
matokeo yaliyoipa ushindi Chadema, Jesca alisema; “mimi binafsi matokeo
ya majimbo yote saba ya uchaguzi mkoani Iringa yakiwemo ya jimbo la
Iringa Mjini nimeyapokea na kama kuna taratibu zingine za kuyapinga
matokeo hayo tufuate sheria.”
Alisema
CCM inatakiwa kufanya tathmini ya kina ya uchaguzi katika jimbo la
Iringa Mjini na mengineyo kwa kutumia vikao halali vya chama ili amani
iliyopo isivurugike kwasababu za majungu.
Alisema
kama kuna malalamiko ya kwenda mahakamani, polisi au kwenye chama,
wanachama wote wa CCM wanatakiwa kutuliza akili na kufuata taratibu ili
wajipange upya kwa ajili ya kukijenga chama hicho na kujiandaa kwa
Uchaguzi Mkuu wa 2020.
Souce-Bongo leaks
Post a Comment