WANACHAMA na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliohusika kwa namna moja ama nyingine kukihujumu chama hicho wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu na kukikosesha ushindi katika kata na majimbo kadhaa, wametakiwa kutafuta pa kwenda kabla ya kufukuzwa uanachama.
Kauli
hiyo imetolewa juzi na Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Tabora Mjini,
Abdulrahman Nkonkota alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara wa wana CCM
kutoka maeneo mbalimbali ya mji huo wa kumpongeza Rais Mteule wa awamu
ya tano, Dk John Magufuli kupitia chama hicho.
Alisema
ili CCM iendelee kupata kibali kwa wananchi na kushika dola ipo haja ya
kusafisha chama kwa kuondoa wanafiki na wasaliti walioko ndani ya
chama.
Alisema
hao kwa kuwa wanadumaza maendeleo ya chama pamoja na serikali huku
akibainisha wazi kuwa wataanza operesheni safisha chama ili kiweze
kutekeleza malengo yake yapatayo 19.
“Naunga
mkono kauli ya Rais wetu Mteule Dk Magufuli ya kuwaondoa wanafiki
katika chama ambao wamerudisha nyuma maendeleo ya chama chetu hali
iliyowafanya baadhi yao kupoteza imani kwa chama chao”, alisema.
Awali
Katibu wa CCM wilaya ya Tabora Mjini, Kameth Ndaghine alisoma tamko la
wana CCM wa wilaya hiyo la kumpongeza Dk Magufuli na mgombea mwenza
Samia Suluhu Hassan kwa kuibuka na ushindi wa kishindo katika uchaguzi
mkuu uliofanyika nchini kote Oktoba 25 mwaka huu.
Alisema
wanaamini uwezo mkubwa walio nao viongozi hao utawavusha Watanzania na
kuwaondoa katika dimbwi la umasikini sambamba na kuongeza ajira kwa
vijana.
Aidha
alimwomba Magufuli mara tu atakapoapishwa ahakikishe anaanza kutekeleza
ahadi zake hasa kwa kujenga mahakama ya mafisadi na kuwachukulia hatua
kali wala rushwa ambao wamelifikisha taifa pabaya.
Ndaghine
alisema pamoja na kuanzisha mahakama ya mafisadi awashughulikie
watumishi wa umma wanaoendekeza uzembe na wale wanaofanya kazi kwa
mazoea ili kurudisha imani kwa Watanzania waliomwamini na kuiamini CCM
hadi kuipa ushindi wa kishindo.
Post a Comment