KATIBU Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni
Sefue ametoa taarifa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk
John Pombe Magufuli amefuta sherehe za uhuru mwaka huu na badala yake,
Desemba 9 itakuwa siku ya usafi nchi nzima ili kuondokana na tatizo la
kipindupindu linaoikabili nchi.
Balozi Ombeni ameongeza kuwa, wakuu wa mikoa na wilaya zote wajiandae kuandaa vifaa vya vya usafi kwa ajili ya shughuli hiyo.
“Rais Magufuli ataangalia bajeti
iliyokuwa imeandaliwa kwa ajili ya sherehe hizo, kisha ataielekeza
kwenye sekta au wizara atakayoona inauhitaji ili zikasaidie kule.
“Haipendezi kusherehekea miaka 54 ya
uhuru huku kipindupindu kikituua, hivyo usafi ni muhimu kwa ajili ya
afya zetu,” alisema Balozi Ombeni.
Hayo yamejiri wakati Balozi Ombeni
alipofanya ziara kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili kukagua mashine za
MRI na zile za CT-Scan na vitanda vilivyonunuliwa kutokana na agizo la
Rais Magufuli kuamuru pesa zilizokuwa zimeandaliwa kwa ajili ya bajeti
ya sherehe za ufunguzi wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano, mjini
Dodoma Alhamisi iliyopita zielekezwe Muhimbili kununua vitanda vya
wagonjwa.
NA DENIS MTIMA/GPL
Kwa mujibu wa Sheria
ya Sikukuu za Kitaifa (The Public Holidays Act, Cap 35) pamoja na Sheria
zingine zinazompa mamlaka Rais kutangaza siku yoyote kuwa sikukuu au mapumziko,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli ameamua kuwa maadhimisho ya Sherehe za Uhuru na Jamhuri zitakazofanyika
tarehe 9 Desemba, 2015, yatumike kwa kufanya kazi.
Kwamba maadhimisho ya
Uhuru ya mwaka huu (2015) yatatumika kama kichocheo cha kujenga tabia ya
kufanya kazi (Uhuru na Kazi) katika Taifa letu. Mheshimiwa Rais ameelekeza
Watanzania wote siku hiyo waitumie kwa kufanya kazi mbalimbali kama vile,
mashambani, maofisini, sokoni, viwandani na usafi wa miji yao katika kutimiza
dhana ya Uhuru na Kazi kwa vitendo.
Aidha, kwa kuwa
Sherehe za Uhuru na Jamhuri huendana na Maandalizi mbalimbali ambayo yanatumia
fedha, kwa kuzingatia kuwa siku hiyo itaadhimishwa kwa kufanya kazi, fedha
zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya sherehe hiyo sasa zitumike kwa shughuli
zingine za kijamii ikiwa ni pamoja na kupambana na maradhi hasa kipindupindu,
kununulia dawa za hospitali, vitanda vya hospitali n.k. kadri kamati za
maandalizi zitakavyoamua.
Ieleweke kuwa sherehe
za Uhuru na Jamhuri ni muhimu katika kuadhimisha kumbukumbu ya uhuru wa nchi
yetu. Hivyo, sherehe hizi zitaendelea kuadhimishwa kila mwaka kama kawaida
kuanzia mwaka 2016.
Gerson
Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa
Mawasiliano, IKULU
1 comments:
Huyu mh. ni noma kweli kwa mwendo huu hatuhitaji upinzani juu ya hilo hongera
ReplyPost a Comment