Mkazi
wa eneo la Duluti wilayani Arumeru mkoani Arusha, Juma Isangu akiwa na
mkewe Janet Tinai pamoja na mwanao, Issa Juma (katikati) wakiangalia
nyaraka mbalimbali nje ya nyumba yao mara baada ya kufukuzwa na kisha
kuvunjiwa nyumba yao wilayani humo na kampuni ya Majembe Auction Mart
kwa amri ya mahakama.
Mkazi
wa eneo la Duluti wilayani Arumeru mkoani Arusha, Janet Tinai
akilalamika mbele ya waandishi wa habari akiwa na baadhi ya vyombo vyake
mara baada ya kuhamishwa kwa amri ya mahakama na kampuni ya Majembe
Auction Mart.
Mkazi
wa eneo la Duluti wilayani Arumeru mkoani Arusha, Juma Isangu akiwa na
mkewe, Janet Tinai wakitafakari nje ya nyumba yao mara baada ya
kuhamishwa na kisha kuvunjiwa nyumba yao na kampuni ya Majembe Auction
Mart kwa amri ya mahakama.
(Picha na moses mashalla).
Mahmoud Ahmad.
SERIKALI
imeombwa kuingilia kati sakata la familia ya Juma Isangu mkazi wa eneo
la Duluti wilayani Arumeru mkoani Arusha kuondolewa na kisha kuvunjiwa
nyumba waliyokuwa wakiishi kwa amri ya mahakama kwa madai haki
haikutendeka.
Familia
hiyo iliondolewa juzi majira ya saa 6:30 mchana na kampuni ya udalali
wa mahakama ya Majembe Auction Mart Ltd tawi la Arusha kwa madai kwamba
waliagizwa na msimamizi wa mirathi wa nyumba hiyo aitwaye,Janeth
Fosbrooke kuwaondoa kwa kuwa hawastahili kuwepo ndani yake.
Akizungumza
mbele ya waandishi wa habari waliofika katika eneo hilo, Isangu akiwa
na mkewe, Janet Tinai pamoja na mtoto wao wa kiume, Issa Juma alisema
alisema kwamba kwa sasa hawaelewi ni wapi wataishi kwa kuwa kitendo cha
kuondolewa katika nyumba hiyo na kisha kutupiwa virago hakikufuata
sheria.
Alisema
kwamba wameondolewa kinyemela ndani ya nyumba waliyokuwa wakiishi bila
taarifa ingawa hapo awali waliwahi kushinda kesi ya mgogoro wa nyumba
hiyo nambari 33 ya mwaka 2011 iliyofunguliwa katika mahakama ya ardhi.
Akielezea
tukio hilo Tinai alisema kwamba mnamo juzi majira ya saa 6;30 mchana
watu wapatao sita ambao walijitambulisha kwamba ni madalali wa mahakama
kutoka kampuni ya Majembe Auction Mart walifika katika nyumba
wanayoishi wakiambatana na askari wa jeshi la polisi na kuwataka kutoka
nje ya nyumba hiyo.
Tinai,alisema
kwamba wakiwa wanajiuliza ndipo watu hao waliingia ndani na kisha
kuanza kutoa baadhi ya mali mbalimbali na kisha kuzipeleka ndani ya lori
mojawapo lililokuwa limeegeshwa nje ya nyumba hiyo na kuacha baadhi ya
vitu nje ya eneo la nyumba hiyo.
Alisema
kwamba na mara walipohoji walijibiwa ya kwamba hawakutakiwa kuendelea
kuishi ndani ya nyumba hiyo kwa kuwa kuna amri kutoka mahakama kuu
inayowataka kuondoka mara moja ndani ya nyumba hiyo .
Hatahivyo,
kwa nyakati tofaiti wanafamilia hao walisema kwamba nyumba hiyo ni
halali kwa kuwa walipewa na marehemu Henry Fosbrooke ambaye alikuwa
mmiliki halali wa eneo hilo tangu mwaka 1980 ambaye aliacha wosia
waliuwasilisha mbele ya mahakama kuu kanda ya Arusha kama moja ya
vielelezo na kisha kukubaliwa.
Hatahivyo,Mwenyekiti
wa kitongoji cha Duluti,Elias Kaaya akihojiwa na waandishi wa habari
katika eneo la tukio alisema kwamba hivi karibuni baadhi ya watu ambao
walijitambulisha kwamba ni madalali wa mahakama kutoka kampuni ya
Majembe Auction Mart walifika ofisini kwao na kuwapa taarifa kuwa
wataendesha zoezi la kumtoa mpangaji aitwaye,Isangu kwenye kitongoji
chake.
Huku
akionyesha barua ya mnamo Novemba 11 mwaka huu yenye KUMB
No,REF.NO.MAM/ARJHF/10/2015 mwenyekiti huyo alidai kwamba watu hao
waliomba uwepo wa usimamizi kutoka ofisi yake kumtoa mkazi huyo na kudai
waliwasilisha pia taarifa kwake na jeshi la polisi wilayani Arumeru.
“Majembe
Auction Mart Ltd madalali ya baraza la ardhi na nyumba (court blockers)
ukiwa msimamizi wa amani kwenye kata yako ya Akheri tunakuomba uwepo
katika zoezi la kumhamisha/kumtoa mpangaji ndugu Juma Isangu aliyekuwa
amepangishwa na marehemu Henry Albert Fosbrooke ambapo kwa sasa
msimamizi wa mirathi aliyeteuliwa m/s Janeth Fosbrooke ndiye ametuteua
kutekeleza zoezi hili la kumtoa mpangaji kwenye nyumba”ilisema sehemu ya
barua hiyo
Hatahivyo,
msimamizi wa mirathi wa nyumba hiyo, Fosbrooke hakuweza kupatikana
kuzungumzia tukio hilo lakini msimamizi wa kampuni ya Majembe Auction
Mart Ltd tawi la Arusha, Suleiman Mdoe alisema ya kwamba wao walifuata
taratibu zote kabla ya kuwahamisha wakazi hao ikiwa ni pamoja na
kubandika notisi ya siku 44 kabla ya zoezi kufanyika.
Post a Comment