Na Georgina Misama-MAELEZO
Mkurugenzi
wa Idara ya Habari Bw. Assah Mwambene amekanusha taarifa za uzushi
zinazosambazwa kwenye baadhi ya vyombo vya habari pamoja na mitandao ya
kijamii kuhusu kifo cha Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Mhe. Benjamin
William Mkapa.
Akiongea
katika mkutano na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam Bw.
Mwambene amesema kuwa Mhe. Rais Mkapa ni mzima na mwenye afya nzuri anaendelea na shughuli zake kila siku kama kawaida.
“Mhe.
Rais Benjamin William Mkapa ni mzima hajafariki, wala haumwi na si
jambo jema kumzushia tukio hilo kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria na
nawasihi msiendelee kusambaza ujumbe huo” alisisitiza Mwambene.
Aidha,
katika mkutano huo Mwambene aliwashukuru wahariri, waandishi wa vyombo
vyote vya habari na mitandao ya kijamii kwa ujumla kwa kuonyesha moyo wa
uzalendo katika kipindi chote ambacho Taifa limekuwa katika mchakato wa
uchaguzi na mpaka sasa ambapo serikali inaendelea na maandalizi ya
sherehe za kuapishwa kwa Rais Mteule wa Awamu ya Tano, Mhe. Dkt. John
Pombe Magufuli.
Mwambene
amesema mpaka sasa maandalizi ya sherehe hizo yanaendelea vizuri, zaidi
ya Marais 15 kutoka nchi mbalimbali wamealikwa baadhi wameshawasili
nchini na wengine wanaendelea kuwasili.
Sherehe
za kuapishwa Rais Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania awamu ya
Tano zitafanyika kesho tarehe Novemba, 5 mwaka huu katika uwanja wa
Uhuru.
on Thursday, November 5, 2015
Post a Comment