Mkurugenzi wa Uendeshaji (NHIF),Eugen Mikongoti akifafanua jambo wakati
akizungumza waandishi wa habari kuhusu kuvunjika kwa uzio wa jengo la
mfuko huo linalojengwa mkoani Mbeya kutokana na kukumbwa na mvua na
upepo mkali, amesema jengo hilo liko salama kabisa ila uzio unaosaidia
kuwakinga wajenzi ndiyo ulioanguka kutokana na upepo huokulia ni
Mkurugenzi wa Masoko na Utafiti wa NHIF,Bw Rehani Athuman.
Mkurugenzi
wa Uendeshaji (NHIF),Eugen Mikongoti akifafanua jambo wakati
akizungumza waandishi wa habari kuhusu kuvunjika kwa uzio wa jengo la
mfuko huo linalojengwa mkoani Mbeya.
Mkurugenzi
wa Masoko na Utafiti wa NHIF,Bw Rehani Athuman akionyesha mchoro wa
jengo hilo kwa waandishi wa habari, kushoto ni Mkurugenzi wa Uendeshaji
(NHIF),Eugen Mikongoti
......................................................................................................
Utangulizi:
Mfuko
wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) hivi sasa unaendelea na ujenzi wa
majengo katika mikoa mbalimbali nchini, kwa lengo la kujitosheleza kwa
majengo ya ofisi na kukidhi mahitaji ya wanachama wake na wadau
wengine.Moja ya mikoa ambayo inaendelea na ujenzi huo ni Mbeya, ambako
Mfuko unajenga jengo la ghorofa kumi na mbili litakalokuwa na nafasi za
ofisi na huduma nyingine ndani yake.
Tukio la Kuanguka kwa jukwaa:
Wakati
shughuli hizo za ujenzi zinaendelea, jana mchana katika hali
isiyotarajiwa mvua iliyoambatana na upepo mkali ilinyesha mjini Mbeya.
Upepo na mvua hizo vilisababisha kuanguka kwa jukwaa la jengo hilo na
kutua juu la paa la jengo la ofisi ya Shirika la Umeme Tanzania
(TANESCO) mkoani Mbeya.
Kuanguka
kwa jukwaa hilo hakukuwa na madhara yoyote kwa maisha ya binadamu, kwa
maana kuwa hakuna mtu aliyepoteza maisha au kupata majeraha. Hata hivyo
tukio hilo lilisababisha taharuki kwa wafanyakazi wapatao hamsini
waliokuwemo ndani ya jengo hilo na hivyo kusababisha kazi kusimama kwa
muda. Aidha tathmini ya awali iliyofanyika katika paa la jengo la
TANESCO lililoangukiwa na jukwaa hilo inaonyesha kuwa paa hilo ilipata
hitilafu ndogo ambayo itafanyiwa marekebisho kwa gharama za Mkandarasi
anayejenga jengo la NHIF.
Hatua za kisualama zilizochukuliwa:
Kama
sheria za ujenzi zinavyoagiza, kabla ya kuanza kwa ujenzi wa jengo hilo
Mkandarasi alishajenga uzio kuzunguka jengo zima ili kuhakikisha kuwa
shughuli za ujenzi hazileti madhara kwa wapita njia au ofisi zilizo
jirani. Umakini wa Mkandarasi huyo katika kuzingatia taratibu za
tahadhari katika shughuli za ujenzi, umewezesha jengo hilo la ghorofa
kumi na mbili kufikia hatua nzuri ya ujenzi bila madhara yoyote kwa
wajenzi wenyewe, wapita njia au ofisi za jirani.
Aidha
kufuatia tukio la Jumatatu 02/11/2015, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya
umeshamwandikia Mkandarasi anayeendelea na ujenzi katika jengo hilo
kuhakikisha kuwa uzio unaozunguka jengo zima unaimarishwa zaidi hususani
wakati huu tunapokaribia kipindi cha mvua za masika ili kuepuka
uwezekano wa madhara yoyote kwa binadamu wakati shughuli za ujenzi
zinaendelea.
Namna Habari ilivyoripotiwa:
Tunapenda
kuufahamisha umma kwamba habari zilizoripotiwa jana na baadhi ya vyombo
vya habari kwamba jengo la NHIF mkoani Mbeya limeporomoka, zilipotosha
ukweli wa tukio hilo, kwani kilichoporomoka siyo jengo, bali ni
jukwaa.Tunapenda kusisitiza kuwa tukio hilo limesabishwa na mvua kubwa
na upepo uliovuma katika mji wa Mbeya, wala siyo uzembe wa Mkandarasi
anayejenga jengo hilo.
Wito kwa Wanachama wa NHIF:
Mfuko
wa Taifa wa Bima ya Afya unawaomba wanachama na wadau wake nchini kote
waendelee kuwa watulivu na kuvuta subira kwani changamoto ya ufinyu wa
ofisi katika mikoa itakuwa imepatwa ufumbuzi baada ya kukamilika kwa
ujenzi wa majengo ya unaoendelea hivi sasa katika mikoa mbali mbali
nchini.
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu,
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.
Post a Comment