WATU 17 wanaodaiwa ni wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Jimbo la Igunga mkoani Tabora wamefikishwa mahakamani kwa mara ya pili wakikabiliwa na shitaka moja la kufanya mkusanyiko usio halali wakati wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, 2015 katika eneo la Halmashauri ya wilaya hiyo.
Awali Mwendesha Mashitaka wa Polisi wilaya ya Igunga, Elimajid
Kweyamba akiwasomea shitaka mbele ya Hakimu wa Mahakama ya wilaya ya
Igunga, Leonard Nkola aliieleza mahakama hiyo kuwa Oktoba 27, mwaka huu
majira ya 5:15 asubuhi katika eneo la Halmashauri ya wilaya washtakiwa
Khadija Hassan, Agnes Kube, Amina Haruna, Samwel Mungo, Edward Samwel,
Hussein Said, Shija Masanja, Alexeda Mark, Pius Mihambo, Lucy Samwel,
Shija Gambi, Rachel Kube, Patricia Maganga, Khadija Midday, Mary Safuni
na Scolastika Kube, walikamatwa.
Ilidaiwa walifanya mkusanyiko wakiwa wamebeba mabango yenye ujumbe
mbalimbali unaomtaka msimamizi wa uchaguzi wa majimbo ya Igunga na
Manonga kutangaza matokeo ya uchaguzi ya urais , ubunge na udiwani.
Mwendesha mashitaka aliendelea kuiambia Mahakama kuwa pamoja na Jeshi
la Polisi kuwaonya zaidi ya mara 10, hawakutii hivyo washtakiwa
walitenda kosa hilo kinyume na kifungu cha sheria 74 (1) (3) 75 sura ya
16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 inayozuia mikusanyiko isiyo
halali.
Baada ya washtakiwa kusomewa mashitaka walikana kutenda kosa hilo,
ambapo mwendesha mashitaka aliieleza Mahakama kuwa upelelezi wa kesi
hiyo umekamilika.
Kabla ya Hakimu Nkola kutoa dhamana kwa washtakiwa alitoa onyo kali
kwa wafuasi wa vyama vyote vya siasa huku akisema Mahakama ni chombo
kinachotetea na kusimamia haki pasipo kujihusisha na upande wowote wa
kichama.
Alitoa kauli hiyo baada ya kuona wafuasi wa Chadema wamevalia mavazi ya
chama hicho huku wakipaza sauti kwa kutamka maneno ya kaulimbiu ya chama
hicho, `People’s Power’ mbele ya Mahakama.
Washtakiwa wote kwa pamoja wako nje kwa dhamana ya Sh 300,000 ikiwa
ni pamoja na mdhamini mmoja. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 16,
mwaka huu itakapoanza kusikilizwa.
Post a Comment