Hamisi akiwa akionesha jiko la kukaushia Tumbaku. |
Kuni hutumika zaidi katika uandaaji wa zao la Tumbaku |
SERIKALI imetakiwa
kuwasaidia wakulima wa zao la Tumbaku katika kupanga bei ili kuepuka mgogoro
kati ya mkulima na mnunuzi.
Wito huo ulitolewa na Wakulima wa Tumbaku katika kata ya Mtanila
wilayani Chunya Mkoa wa Mbeya walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari
kuhusianaa na changamoto zinazowakabili.
Wakulima hao wameiomba
serikali kuingilia katika upangaji bei wa zao hilo badala ya kumwachia mkulima
kupanga bei na mnunuzi pekee kwani kuna upande unaonewa.
Wakulima hao walisema
kwa serikali kujiondoa kwenye usimamizi wa bei ya zao hilo kunasababisha
wakulima kunyonywa kwa wanunuzi kujipangia bei zilizo na maslahi yenye kuegamia
upande wao.
Akibainisha hali hiyo, Mwenyekiti
wa Chama cha msingi cha wakulima wa Tumbaku katika kijiji cha Igangwe, kata ya
Mtanila(Igangwe Amcos) Gulila Mwakosya alisema wakulima wanaamini wananyonywa
kwakuwa mara zote wanunuzi wamekuwa wakinunua kwa bei wanayoijua wao wakisema
ndiyo inayoendana na soko la kimataifa.
Mwakosya alisema ni vigumu
kwa mkulima kutokubaliana na bei inayopendekezwa na mnunuzi kwakuwa ni mtu wa
chini asiyeweza kujua bei ya tumbaku katika soko la kimataifa.
Alisema kwa serikali
kuingilia kati upangaji bei ya tumbaku itawezesha pande zote mbili kunufaika
kwa usawa kwakuwa yenyewe ina uwezo mkubwa wa kutambua bei ya zao hilo katika
soko la dunia.
Aliongeza kuwa endapo
Serikali itapanga bei mnunuzi hata kuwa na nafasiya kujiamlia badala yake
atafuata bei elekezi ambayo itaendana na ongezeko la bei ya pembejeo za kilimo
pamoja na gharama za kuhudumia zao hilo.
Kwa upande wake mmoja wa
wakulima wa kijiji cha Igangwe, Hamis Mwandura, alisema serikali pia
inapaswa kusimamia wanunuzi kuendeleza utaratibu wa kukutana na wakulima wa zao
hilo mara kwa mara na kujadiliana kwa pamoja mambo yenye kuleta ushirikiano
endelevu.
Alisema gharama za
kuandaa shamba, kusia mbegu, kupandikiza na kuanza kuhudumia miche gharama yake
ni kubwa lakini kipindi cha mavuno wanunuzi huja na bei zao bila kujali mkulima
alitumia shilingi ngapi.
Credit: Mbeya Yetu Blog
Post a Comment