Wanachama
115 wa Chadema na CUF wilayani Handeni Mkoa wa Tanga, wamejiunga na CCM
kwa madai kuwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) umeshindwa kuelewana
hadi kipindi cha Uchaguzi Mkuu.
Wakirudisha
kadi na bendera juzi mbele ya Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Tanga,
Mathew Mganga walisema walikuwa na nia ya kweli ya kuunga mkono Ukawa
unaoundwa na vyama vyao lakini kutokana na kutokuwa na msimamo wameamua
kuhama.
Katibu
wa Chadema Kata ya Kwenjugo, Rajabu Vuli, alisema alifanya hamasa
kuhakikisha chama chao kinapata ushindi lakini viongozi wa wilaya
hawakuonyesha ushirikiano na watu wa chini.
Mwingine aliyehama ni Katibu wa Vijana wa Chadema wa kata hiyo, Ramadhani Dawa.
Dawa alisema ahadi zisizotimia za viongozi ikiwamo kuwadharau viongozi wa kata ndiyo sababu kubwa iliyosababisha kuhamia CCM.
Alisema
kama wasingedharauliwa na mawazo yao kufanyiwa kazi wangebaki Chadema
na kukiendeleza chama hicho ambacho amedai kimekuwa na mvuto mkubwa na
Watanzania ambao walitaka kuleta mabadiliko ya kweli.
Mganga alisema wamepokea wanachama hao bila wasiwasi kwani tayari hizo ni kura.
Hivi sasa chama hicho kipo kwenye kampeni za kumuombea kura mgombea ubunge Jimbo la Handeni Mjini (CCM), Omari Kigoda.
Alisema wameridhika na uamuzi wa wanachama hao wapya kwa kuona CCM inajali ngazi zote za uongozi kuanzia wa chini hadi juu.
Alisema
baada ya uchaguzi huo mdogo, watahakikisha yale walioahidi kwa wananchi
yanafanyiwa kazi haraka hasa yanayowagusa moja kwa moja ikiwamo elimu,
afya, maji na masuala ya miundombinu.
Mgombea ubunge huyo, aliahidi endapo atapewa ridhaa ya kuongoza jimbo hilo, atawaleta maendeleo.
Post a Comment