Mkuu wa
Wilaya ya Kinondoni Paul Makonda akiongea na baadhi uongozi wa Mamlaka ya Maji
Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASA) na viongozi wa ulinzi na usalama
wilaya ya Kinondoni kabla ya kuanza ziara yake ya kujionea hatua zilizofikiwa
kwenye mradi wa upanuzi wa mtambo wa Ruvu Juu, ulazaji wa bomba kuu la maji
kutoka Mlandizi hadi Kimara, ujenzi wa tanki jipya la Kibamba na kukarabati
matenki ya maji Kimara mwishoni mwa wiki jijini Dar es salaam.
Mkuu wa Wilaya ya
Kinondoni Paul Makonda (wa kwanza kushoto) akiwa na baadhi viongozi wa Mamlaka
ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASA) na viongozi wa ulinzi na
usalama wilaya ya Kinondoni walipotembelea na kujionea maeneo yaliyojengwa kuzunguka
matenki ya maji Kimara mwishoni mwa wiki jijini Dar es salaam. Wa kwanza kulia
ni Meneja wa Miundombinu Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam
(DAWASA) Mhandisi John Kirecha.
Mkuu wa Wilaya ya
Kinondoni Paul Makonda (wa pili kulia) akiwa na Meneja Uhusiano wa Jamii wa
Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es salaam (DAWASA) Bi.Neli Msuya (wa pili
kushoto) pamoja na baadhi viongozi wa Mamlaka hiyo na viongozi wa ulinzi na
usalama wilaya ya Kinondoni walipotembelea na kujionea nyumba na makazi ya watu
yaliyojengwa kuzunguka matenki ya maji Kimara mwishoni mwa wiki jijini Dar es
salaam. Wa kwanza kulia ni Meneja wa Miundombinu Mamlaka ya Maji Safi na Maji
Taka Dar es Salaam (DAWASA) Mhandisi John Kirecha na Meneja DAWASA tawi la
Kimara Bw. Robert Mugabe (wa kwanza kushoto).
Mkuu wa Wilaya ya
Kinondoni Paul Makonda akiingia ndani ya eneo linapojengwa tanki jipya la maji eneo
la Kibamba ambalo litakuwa uwezo wa ujazo wa lita milioni 10 kwa siku na
kujionea shughuli za ujenzi huo unavyoendelea wakati wa ziara yake mwishoni mwa
wiki jijini Dar es salaam.
Mkuu wa Wilaya ya
Kinondoni Paul Makonda na msafara wake wakiwa eneo linapojengwa tanki jipya la
maji eneo la Kibamba ambalo litakuwa uwezo wa ujazo wa lita milioni 10 kwa siku
na kujionea shughuli za ujenzi huo unavyoendelea wakati wa ziara yake mwishoni
mwa wiki jijini Dar es salaam.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Paul Makonda (katikati) akiongea na viongozi wa
kampuni ya MEGHA kutoka nchini India ambao ndiyo wanajenga mradi wa bomba la
maji kutoka Ruvu Juu pamoja na tanki la maji linalojengwa Kibamba. Wa pili
kulia ni Meneja wa kampuni ya MEGHA Mohan Dendkri.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Paul Makonda na msafara wake wakiwa eneo la Kibamba
Luguruni kujionea mabomba yanayotumika katika ujenzi wa mradi wa maji wa Ruvu
Juu yalipozuiliwa na kuzungushiwa uzio kitu ambacho kinakwamisha kukamilika kwa
ujenzi wa mradi huo kwa wakati.
Baadhi ya mabomba
yakiwa ndani ya uzio.
(Picha na Eleuteri
Mangi –MAELEZO)
Na Eleuteri Mangi -
MAELEZO
Mkuu wa Wilaya ya
Kinondoni Paul Makonda ameuagiza uongozi wa
Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASA) kuandaa orodha
ya wananchi waliojenga juu ya miundo mbinu ya maji na kuipeleka orodha hiyo ofisini
kwake kwa hatua zaidi.
Akiongea na uongozi wa
DAWASA mwishoni mwa wiki baada ya kuhitimisha ziara yake ya kujionea hatua
zilizofikiwa kwenye mradi wa upanuzi wa mtambo wa Ruvu Juu, ulazaji wa bomba
kuu la maji kutoka Mlandizi hadi Kimara, ujenzi wa tanki jipya la Kibamba na
kukarabati matenki ya maji Kimara, Makonda alisema kuwa nia ya Serikali kuwapa
huduma ya maji wananchi kwa wakati.
“Nataka kazi hii ya
ujenzi wa mradi wa bomba la maji ukamilike kwa muda ulivyopangwa uweze
kuwaondolea wananchi kero ya maji inayowasumbua, huduma ya maji ni ya muhimu
sana kwa wakazi wa Dar es salaam, upatikanaji wake utasaidia kupunguza magonjwa
mengi hasa ya milipuko ambayo ni hatari kwa afya wananchi wetu” alisema
Makonda.
Agizo la Mkuu huyo wa
Wilaya linafuatia kuwepo kwa vikwazo mbalimbali vinavyochelewesha mradi wa
ujenzi wa bomba hilo kukamilika kwa wakati katika maeneo ya Kimara yalipo
matangi ya maji ambapo makazi ya watu yamejengewa kuzunguka matangi hayo na
kuhatarisha usalama wa maisha ya wakazi hao na usalama wa miundombinu ya maji.
Eneo lingine ambalo
limekuwa kikwazo cha kukamilisha mradi huo ni Kibamba Luguruni ambapo mabomba
ya mradi yamezuiliwa kwa kufungiwa na kuzungushiwa kwenye uzio na mkazi wa eneo
hilo Bw. Enock E. Mwakassala.
Kwa mujibu wa DAWASA,
mkazi huyo hana uhalali wa kumiliki eneo hilo maana amevamia eneo la Wakala wa
Barabara Tanzania (TANROADS) kwa sababu zake binafsi na hivyo kuchelewesha
ujenzi wa mradi.
Aidha, Makonda
ameuagiza uongozi wa DAWASA kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania
(TANESCO) kuwaainisha watu wote waliojenga ndani ya hifadhi ya eneo la miundombinu
ya shirika hilo ambalo limetoa sehemu ya hifdhi yake kwa lengo la kujenga na
kulaza bomba jipya la kusambaza maji kutoka Mlandizi hadi Kimara yalipo matangi
ya kusambazia maji ambayo yatawanufaisha wakazi wa maeneo mbalimbali ya jiji
hilo.
Kwa upande wake
Mhandisi Msimamizi wa Mradi huo kutoka DAWASA Christian Christopher amesema
kuwa mradi huo wa ujenzi wa bomba la maji kutoka Ruvu Juu una jumla ya km 69
ambapo hadi sasa km 46 ujenzi wake tayari umekamilika na zimebakia km 23 ambazo
zinatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Januari 2016.
Mhandisi Christian
alisema kuwa mradi wa ujenzi wa bomba la maji kutoka Ruvu Juu unatekelewa na
kampuni ya MEGHA kutoka nchini India inayoongozwa na Meneja wake Mohan Dendkri chini ya makubaliano ya kandarasi Na.
AE/033/2012-13/WC/25.
Vile vile Mhandisi
Christian aliongeza kuwa kutoka eneo la Mlandizi ambalo ndiyo chanzo cha maji
yanapotoka yatasafirishwa kwa bomba lenye kipenyo cha ukubwa mm 1200 hadi
Kibamba ambapo linajengwa tangi la maji lenye uwezo wa ujazo wa lita milioni 10
kwa siku na baadaye maji hayo kusafirishwa hadi Kimara, kipenyo cha bomba la
kutoka Kibamba hahi Kimara ni mm 1000 na kutoka Tanita hadi Kibamba bomba hilo
lina kipenyo cha mm 900.
Wakazi wa jiji la Dar
es salaa asilimia 25 wanategemea maji kutoka chanzo cha Ruvu Juu na asilimia 75
wanapata maji kutoka chanzo cha maji kutoka Ruvu Chini. Mtambo wa
Ruvu Juu unahudumia
wakazi wa Mlandizi,
mji wa Kibaha na
maeneo ya Kiluvya, Mbezi,
Kimara, Ubungo, Tabata
na Segerea. Mtambo
wa Ruvu Chini unahudumia maeneo
ya Mji wa Bagamoyo, Bunju. Boko, Mbezi Beach, Kawe, Kinondoni, katikati ya
Jiji, Sinza, Magomeni,
Buguruni, Ilala na
Keko. Mtambo wa
Mtoni unahudumia maeneo ya
Temeke, Tandika, Kurasini,
baadhi ya maeneo
ya Keko na
Mbagala.
Post a Comment