Nawasalimu
nyote katika jina la nchi yetu Tanzania,
Mimi ndugu yenu sijambo, naendelea kusukuma mbele gurudumu la maendeleo
kujenga nchi yetu. Nawapongezeni sana kwa ushindi mkubwa mlioupata
ambao leo umewawezesha kutuwakilisha Watanzania wote katika Bunge la
Jamhuri ya Muungano, muhimili namba mbili katika nchi yetu.
Najua mmepita katika safari ndefu, wengi wenu mna majeraha, hayo yote
yamepita, sasa ni kazi moja tu; kuwawakilisha vyema wananchi waliowatuma
ili
muweze kulisogeza taifa letu mbele kwa kuisimamia vyema serikali na
zoezi zima la utungaji wa sheria.
Nawapongezeni
sana kwa uchaguzi wa Spika Mheshimiwa Job Ndugai, Naibu Spika
Mheshimiwa Dk. Tulia Mwansasu na pia Mheshimiwa Waziri Mkuu wa
10 wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Majaliwa Kassim
Majaliwa. Hongereni sana.
Najua mtawakumbuka sana wabunge wenzenu ambao hawakupata nafasi ya
kurejea bungeni, kama David Kafulila, kijana aliyejitolea kwa nguvu zake
zote
na hata kuhatarisha maisha yake mwenyewe katika Sakata la Escrow, lakini
wananchi wa jimbo lake wakamuona alikuwa mbunge wa taifa si mbunge wao,
wakamkata.
Pia
mtawakumbuka sana wabunge walioaga dunia kama Deo Filikunjombe, Dk.
Abdallah Kigoda, Celina Kombani, Kapteni John Komba, Mariam Mfaki,
Clara Diana Mwatuka, Mungu azilaze roho zao mahali pema peponi, ni vyema
mkasimama hata kwa dakika moja kuwakumbuka na ninamwomba Mungu
wa Mbinguni, atuinulie watu wengine kama wao katika Bunge hili,
watakaokuwa tayari kusimama kidete kutetea maslahi ya wanyonge.
Baada
ya kusema hayo nielezee dhumuni la kuwaandikia barua yangu, kwani
imekuwa ni desturi yangu sasa kuandika barua moja kila wiki, naandika
barua hii kuwakumbusheni juu ya jukumu lililowapeleka Dodoma na
matarajio ya wananchi waliowatumeni kazi, najua mnafahamu lakini si
jambo
baya kukumbushana ili asiwepo mtu atakayedhani amekwenda Dodoma kufaidi
maisha, akabweteka kwa sababu ya heshima anayoipata hivi sasa kama
mbunge, miaka mitano si karne, 2020, mtakutana na wananchi kwenye boksi
la kura, yasije yakawapata yaliyowapata ambao hawakurejea.
Ndugu
zangu waheshimiwa wabunge wa Jamhuri ya Tanzania,
Mmepata bahati ya kuwa wabunge wa kwanza wa Bunge la 11 la awamu ya tano
chini ya Rais Dk. John Pombe Magufuli, mmeupata ubunge katika kipindi
ambacho uchumi wa nchi yetu katika robo ya pili ya mwaka 2015 unakuwa
kwa kasi ya asilimia 7.9, hii ni kasi nzuri kwani kuanzia mwaka 2002
-2014
uchumi wa taifa hili hili ambao ninyi ni wabunge wake ulikuwa ukikua kwa
wastani wa asilimia 6.72.
Waheshimiwa wabunge,
Wakati uchumi wa nchi yetu ukikua kwa asilimia 7.9, nchi nyingi za
Afrika zinasuasua sana nyuma yetu, kasi ya ukuaji wa uchumi wetu kwa
mujibu
wa taarifa za benki ya dunia umezidi mataifa makubwa duniani kama China
ambayo uchumi wake umekuwa kwa asilimia 6.9 tu!
Na
India ni asilimia 7,
kwangu mimi hii ni dalili nzuri inayonyanyua matumaini yangu kwamba,
hata kama hali ni mbaya hivi sasa, kama serikali itasimamiwa vizuri na
Bunge
ambalo ninyi ni wabunge wake, hakika tumekaribia kufika katika nchi ya
ahadi.
Kwa nini nimeamua kuwaandikia barua hii? Waheshimiwa wabunge, pamoja na
takwimu zote zilizoko hapo juu ambazo zinaashiria mema huko
tuendako, ni ukweli ulio wazi kwamba ukuaji wa uchumi wetu haujaonekana
kwenye meza ya chakula na maisha ya Mtanzania wa kawaida.
Katika nchi yetu yenye jumla ya watu wasiopungua milioni 48, milioni 12
kati yao bado wanaishi katika umaskini mkubwa, hizi ni takwimu za mwaka
2015!
Huduma
za afya bado ni mbaya, watu wengi wanakufa kwa magonjwa yanayoweza
kutibika, elimu yetu bado ni duni, watumishi wetu wa umma bado
hawalipwi vizuri na wamevunjika moyo, huduma za maji na umeme vijijini
bado ni duni, vifo vya akina mama na watoto bado viko juu.
Sarafu yetu inazidi kuporomoka, imeshuka kwa karibu asilimia ishirini
ikilinganishwa na thamani ya dola ya Kimarekani!
Jambo
ambalo limesababisha
kupanda katika bei ya vitu vinavyoagizwa nje ya nchi na kufanya mfumuko
wa bei ambao mwaka 2011 ulikuwa asilimia 20 ukashuka mpaka asilimia 4 ,
Juni 2015, upande tena mpaka asilimia 6.4 jambo ambalo limechangiwa pia
na kupanda kwa vyakula.
Waheshimiwa wabunge mnaingia bungeni Tanzania ikiwa na tatizo kubwa sana
la ajira, takwimu zikionyesha kwamba karibu nguvu kazi ya vijana
800,000 huingia sokoni kila mwaka, soko ambalo halina ajira kwa ajili
yao!
Hili
ni tatizo kubwa sana kwa taifa kama Tanzania ambalo vijana wake wengi
wametegemezwa kuwa mara wamalizapo vyuo (ambazo hivi sasa ni vingi kila
kona ya nchi) kutakuwa na ajira za kuwapa.
Nawaandikieni barua hii kuwakumbusheni ndugu zangu juu ya jukumu kubwa
mlilonalo kwa taifa na watu wenu, hakika haiko sababu ya ninyi
kusherehekea
kuwa wabunge, kwani ushindi wenu ndiyo mwanzo wa kazi kubwa mliyonayo
mbele, ambayo kwa mtu mwenye uzalendo wa kweli kwa taifa lake ubunge
ni mzigo.
Najua
mmeingia Bungeni kwa kupitia vyama mbalimbali, wengine mmeteuliwa,
najua mnazo tofauti mbalimbali, zikiwemo za dini, rangi, kabila
na itikadi, nawaombeni sasa muweke tofauti zenu zote pembeni na kusimama
pamoja kama wawakilishi wa watu ili kuisimamia Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania vyema iweze kutimiza majukumu yake.
Kuendelea
kusimama na U-CCM, U-Chadema, U-Cuf, U-NCCR MAGEUZI, hakika
hakutaisaidia lolote Tanzania yetu na watu wake, hivi sasa ninyi ni
wawakilishi wa Watanzania, simamieni maslahi ya watu wa taifa hili na
maslahi ya taifa kwa ujumla wake.
Mnapoingia bungeni katika kipindi hiki ambacho taifa letu linakabiliwa
na hali ngumu ya uchumi, kukiwa hakuna fedha za kutosha kujiendesha, si
jambo jema hata kidogo kuendelea kugawanyika, umoja peke yake ndiyo
utaweza kubadilisha mambo.
Najua
ninyi nyote ni wazalendo kwa taifa lenu,
basi uonyesheni uzalendo wenu kwa vitendo ili kuhakikisha uwepo wenu
Bungeni kwenye Bunge la 11 unakuwa ni wa kihistoria, wengi wenu ni
vijana,
matarajio yangu ujana, elimu na vipaji mlivyonavyo mtavitumia vizuri
katika kuhakikisha vipaumbele vya taifa hili vinaandaliwa vyema kwa
faida ya
waliopo na watakaofuata baada ya sisi.
Nasi tulioko huku nje ya Bunge hatutawaachia mzigo huu peke yenu,
tutatimiza wajibu wetu kama Watanzania wawajibikaji.
Tutapiga
kelele kila
tutakapoona mambo hayaendi sawa, ufisadi unafanyika hadharani na
rasilimali za taifa hili zinatumiwa na watu wachache kwa faida yao wao
na familia
zao, huu kwetu utakuwa ni uzalendo kwa taifa ambalo tumeapa kulitetea
wakati wote na kuvitetea vyama vyetu pale tu vinapostahili.
Tanzania inasonga mbele, ilipo leo ni bora kuliko ilikokuwa jana, kama
uchumi wetu ukiendelea kukua jinsi unavyokua kwa kasi, nina uhakika
tutawapita
waliokuwa mbele yetu wakiwa wamekaa! Hili halitakuja kama zawadi bali
matokeo ya matendo yetu mema tutakayoyafanya, ninyi Bungeni na sisi huku
nje ya Bunge, sote tuna wajibu wa kujenga taifa letu.
Baada
ya kusema haya niwatakieni bunge jema lenye mafanikio na nimtakie
Mheshimiwa Spika Job
Ndugai hekima na Busara za kuliendesha bunge hili vizuri, vivyo hivyo
kwa msaidizi wake, pia waziri mkuu wetu mpya ambaye ni msimamizi wa
shughuli
zote za serikali Bungeni, namtakia kila la kheri.
Mungu ibariki Tanzania,
Mungu libariki Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wabariki wabunge wote na wape moyo wa kizalendo na hekima za kuwafikiria
wananchi wa taifa hili katika maamuzi yao.
Wasalaam,
Eric Shigongo James
...............................................
BARUA KALI
Post a Comment