BARAZA LA TAIFA LA UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI
MKUTANO WA WADAU WA UWEZESHAJI UTAKAOFANYIKA TAREHE 9/02/2016.
Baraza
la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) lilianzishwa mwaka 2005
kwa Sheria ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (Sheria na. 16 ya
Mwaka 2004) chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Baraza ni chombo cha juu
kitaifa cha kuratibu, kusimamia, kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa
Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya mwaka 2004.
Katika
kutekeleza Sera ya Taifa ya Uwezeshaji, Baraza limeshaandaa Mkakati wa
Taifa wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Mwongozo wake unaohusisha sekta
zote nchini.
Ili
kufanikisha utekelezaji wa mkakati huo, Baraza limeandaa Mkutano wa
Wadau wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ambao ni muundo rasmi katika
kutekeleza Mkakati wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi. Mkutano huu ni
sehemu ya Uratibu na utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji ambao
unahusisha wadau mbali mbali ambao ni Wizara, Idara na Taasisi za
Serikali, Mamlaka za Serikali za Mitaa, mashirika yasiyo ya kiserikali
na sekta binafsi.
Mkutano
huu wa Wadau wa Uwezeshaji utafunguliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mh Majaliwa Kassim Majaliwa (MB), tarehe 9/02/2016
katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere.
MAJUKUMU YA BARAZA
i. Kuandaa Mpango Mkakati wa Kisekta na kuhamasisha matumizi ya rasilimali kwa shughuli za uwezeshaji wananchi;
ii. Kuhamasisha na kuhimiza uwekaji wa akiba, uwekezaji na ushirikishwaji makini wa wananchi kwenye shughuli za kiuchumi;
iii. Kusimamia, kuongoza na kubaini vyanzo vya fedha kwa ajili ya Mfuko wa udhamini mikopo ya uwezeshaji ;
iv. Kuwezesha
na kuratibu mafunzo ya ujasiriamali kwa vikundi mbalimbali vya wananchi
kutegemeana na mahitaji na changamoto zinazowakabili;
MALENGO YA MKUTANO WA WADAU WA UWEZESHAJI
- Kukutanisha wadau wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kutoka sekta za umma na binafsi hapa nchini,
- Kujadili taarifa ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi;
- Kutambua juhudi za wadau wanaotekeleza Sera ya Taifa ya Uwezeshaji;
- Kujaidili changamoto na kuibua mbinu bora za utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi;
- Kuhamasisha juhudi mbali mbali za Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi,
MATARAJIO
Kupitia Mkutano huu wa Wadau wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Baraza lina matarajio yafuatayo;
i. Kuanza
rasmi kwa Dawati la Uwezeshaji na Ushiriki wa Wananchi kuanzia ngazi
ya Wilaya, Mkoa, Wizara na Idara katika kufuatilia masuala ya
Uwezeshaji, kuandaa taarifa na kuwasilisha katika kamati husika kwa
maafikiano na kuwasilisha katika Baraza la Taifa la Uwezeshaji;
ii. Taasisi
za umma na binafsi kuwahudumia wananchi kwa ufanisi bila upendeleo pale
wanapohitaji kuwezeshwa kupitia huduma wanazozitoa katika utendaji wao
wa kila siku;
iii. Kuratibu majukumu ya Uwezeshaji kwa kuzingatia uwajibikaji, uadilifu, uaminifu na kujali;
iv. Kuchochea
hamasa na kuhakikisha kuwa wananchi wanapewa upendeleo wa pekee kwa
watoa huduma mbalimbali katika zabuni na miradi mikubwa katika maeneo
yao pale wanapokidhi vigezo na masharti ya zabuni husika.
v. Kila
kiongozi kuhakisha kuwa rasilimali zilizotengwa kwa ajili ya kutekeleza
miradi mbalimbali ya kiuwezeshaji wananchi kiuchumi zinaelekezwa katika
miradi hiyo na kutumika kwa kuzingatia thamani ya pesa na miradi
yenyewe;
Baraza
linapenda kuwashukuru wadhamini wa Mkutano huu ambao ni (Mradi wa
Ushindani wa Sekta Binafsi (Private Sector Competitiveness Project),
World Vision Tanzania, Benki ya Maendeleo ya TIB (TIB Development Bank),
Benki ya Posta, Benki ya CRDB, UTT Microfinance, Mfuko wa Pensheni wa
Watumishi wa Umma (PSPF), Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Serikali za
Mitaa (LAPF), Mfuko wa Mafao ya Kustaafu (GEPF) na Shirika la Nyumba la
Taifa (NHC).
Post a Comment