SERIKALI
imezungumzia umuhimu wa kulifufua upya Shirika la Ndege nchini Air
Tanzania (ATC) kwa kulinunulia ndege mpya na kulipa mtaji ili lifanye
kazi kibiashara na kutengeneza faida kama ilivyokusudiwa awali.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa
(Pichani)ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na menejimenti na
wafanyakazi wa Shirika hilo alipolitembelea jijini Dar es Salaam leo.
“Tutawekeza
kwenye Air Tanzania ili kuongeza fursa za kiuchumi na kuvutia wasafiri
wengi kufika nchini moja kwa moja na kuvutia sekta ya utalii”, amesema
Waziri Prof. Mbarawa.
Waziri
Prof. Mbarawa amewataka wafanyakazi wa Shirika hilo ambao sio waadilifu
na wavivu kuondoka mara moja ili kupisha wafanyakazi wabunifu na wenye
mawazo ya kibiashara kuendesha shirika hilo kwa faida.
“Tunataka
watu watakaolitoa shirika hili kutoka sehemu moja hadi nyingine kwa
kuliwezesha kiuchumi na kujitegemea ili kushindana na mashirika mengine
ya ndege katika biashara“, amesisitiza Prof. Mbarawa.
Prof.
Mbarawa amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John
Magufuli yuko tayari kununua ndege mpya ili kulifufua shirika hili hivyo
amewataka wafanyakazi hao kuwa na mtazamo chanya wa kufanya biashara
ili kuiletea taifa tija.
Kwa
upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa ATC Bw. Johnson Mfinanga
amemwambia Waziri Prof. Mbarawa kuwa kwa sasa shirika hilo lipo katika
hali mbaya kiuchumi na hivyo kuhitaji nguvu ya Serikali kulikwamua ili
litoe huduma inayoshahili.
Aidha,
Waziri Prof. Mbarawa amesisitiza kuwa Serikali itaangalia upya taratibu
za ajira katika shirika hilo na watakaobainika kuajiriwa kinyume cha
taratibu watafukuzwa kazi mara moja.
“Tutanataka
watu waadilifu, wabunifu na wenye sifa stahiki ili wafanye kazi kwa
maslahi ya shirika na taifa kwa ujumla”, amefafanua Waziri Mbarawa.
Shirika
la Ndege nchini ATC toka mwaka 2009 limekuwa likijiendesha kwa hasara
na Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kulifufua shirika hilo ili
lifanye kazi kwa faida na kuboresha usafiri wa anga ndani na nje ya nchi
na hivyo kuvutia wasafiri wengi kuja nchini moja kwa moja.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Post a Comment