Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini Mhe. JaJi Francis S.K. Mutungi amevitaka vyama vya Siasa nchini kuhakikisha kuwa Katiba na Kanuni za Vyama vya Siasa zinaheshimiwa na kufuatwa katika utendaji wa kila siku wa chama cha siasa ili kuepuka migogoro na migongano ndani ya vyama. Hayo ameyabainisha kwenye barua yenye Kumb. Na. HA.322/362/01/103 aliyoiandikia vyama vya siasa mapema leo.
“Nimeona ni vyema nitumie fursa hii kuviasa Vyama vya Siasa kuhusu hali hii, kwani hali hii ya kufanya mambo kiholela pasipo kufuata Katiba na Kanuni kama itaachwa iendelee hivi ndani ya vyama kwa hakika italeta migogoro na mipasuko mikubwa ndani ya Vyama vya Siasa husika.”
“Wakati huu ambapo nchi yetu inasubiri marudio ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar, nimeandikiwa barua na pia kupata nakala za barua kutoka kwa baadhi ya Vyama vya Siasa kuhusu migongano ya wanachama na viongozi au viongozi wenyewe kwa wenyewe kuhusu suala la kushiriki uchaguzi wa marudio Zanzibar. “alisema Jaji Mutungi
Barua hiyo ilibainisha kuwa suala hilo la migongano limejitokeza pia kwa wingi kwenye Vyombo vya Habari, ambapo wanachama na viongozi au viongozi wenyewe kwa wenyewe wametofautiana na kupingana hadharani.
Jaji Mutungi amesema kwa mujibu wa Kanuni ya 3(1) ya kanuni za Usajili wa Vyama vya Siasa za mwaka 1992 (GN.No. 111) Vyama vya Siasa vinaposajiliwa vinapaswa kuwasilisha Katiba na Kanuni zake kwa Msajili wa Vyama vya Siasa.
“Ikumbukwe kwamba, suala la msingi hapa ni kwamba,sharti la kuwepo kwa Katiba na Kanuni katika chama, kimsingi ni mwendelezo wa kukuza na kudumisha dhana ya kuendesha Vyama kitaasisi kulingana na mwongozo uliokubalika na kuasisiwa kichama kwa mfumo wa Katiba na Kanuni za chama na si kuendesha chama kiholela kama inavyoelekea kuota mizizi kwa baadhi ya Vyama vya Siasa hivi sasa.”ameongeza Jaji Mutungi
Jaji Mutungi amevisihi Vyama vyote vya Siasa, kuhakikisha kwamba matamko ya chama hususan yahusuyo msimamo wa chama kuhusu jambo zito la kisera, kitaifa n.k., mathalan kama lilivyo la uchaguzi huu wa Zanzibar basi yatolewe rasmi na mtu mwenye mamlaka ya kuongea kwa niaba ya chama. Na endapo kuna mwananchama au kiongozi ambaye ataenda kinyume achukuliwe hatua haraka iwezekanavyo na chama husika kwa kuzingatia katiba na kanuni zake ili kuepusha sitofahamu inayokuwa imejitokeza katika jamii.
“Ni vyema misimamo kama hiyo ya chama itokane pia na vikao halali vya chama na siyo matakwa ya kiongozi mmoja au mwanachama mmoja au wachache. Vinginevyo kama tutapeleka na kufanya uendeshaji wa vyama kiholela tutachangia kuwachanganya wananchi na kupoteza kabisa imani na heshima ya Jamii iliyokuwa imeanza kujengeka kwa Vyama vya Siasa”. Amesisitiza Jaji Mutungi
Aidha vyama vvya Siasa vimeaswa kuchua hatua ya haraka iwezekanavyo kwa mwanachama au kiongozi wa chama anayefanya mawasiliano ama kutoa matamko bila idhini ya mamlaka na pia vyama vimeonywa kutowajengea wananchi tashwira ya kwamba kuna makundi yanagombania madaraka na kuendeleza maslahi binafsi kwa sababu jambo hilo linashusha hadhi ya vyama vya Siasa nchini.
Post a Comment