Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

MWANAHARAKATI DK. BISIMBA ASHANGAZWA NA AJALI YAKE

Licha ya kwamba kwa sasa hawezi kutembea mwenyewe, anakula akiwa kitandani, anaamini ipo siku hali yake itarejea kama ilivyokuwa awali.

Novemba 8, mwaka jana , saa tatu asubuhi, Dk Hellen Kijo Bisimba alipata ajali ya gari katika barabara ya Ali Hassan Mwinyi, eneo la mataa ya Agha Khan wakati akielekea kanisani Kurasini.

Dk Bisimba ni Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) ambacho kimekuwa kikiisaidia jamii kwa huduma za kisheria.

Katika ajali hiyo, gari lake liligongwa na kupinduka mara nne na kulikuwa na watu wanne lakini baada ya gari hilo kupinduka Dk Bisimba ndiye aliyeumia zaidi sehemu mbalimbali za mwili wake, ikiwamo kuvunjika mguu na bega.

Baada ya ajali hiyo Dk Bisimba alipelekwa Hospitali ya Aga Khan kwa ajili ya matibabu kisha baadaye kuhamishiwa katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (Moi).

Hata hivyo, Moi walimpa rufaa ya kwenda India, kwa ajili ya matibabu zaidi.

Dk Bisimba amerejea nchini baada ya matibabu India yaliyomchukua karibu miezi mitatu.

Itakumbukwa kuwa Dk Bisimba alipelekwa India bila kupata fursa ya kuelezea umma juu ya jinsi ajali hiyo ilivyotokea pia kwa sasa wengi watapenda kujua hali yake kiafya iko namna gani.


Hali yake kwa sasa
Dk Bisimba anasema baada ya matibabu India kwa sasa anaendelea vyema licha ya kwamba hawezi kutembea mwenyewe bila kuwa na usaidizi wa mtu au magongo.

Pamoja na hali hiyo, anasema anaendelea vizuri na hali yake inaendelea kuimarika.

Anasema kuna mambo ya kiofisi ambayo anaweza kuyafanya ikiwamo kusoma ripoti na kutia saini kama Mkurugenzi Mtendaji wa LHRCR.

Kuhusu mambo ambayo kwake ni vigumu kwa sasa kuyafanya, anasema “Kuna mambo kama suala la kuoga, siwezi kufanya nikiwa peke yangu hadi nipate msaidizi. Siyo hilo hata chakula, siwezi kukifuata au kwenda kukaa mezani. Huwa naletewa hapa kitandani na kula. Nina uwezo wa kutumia mikono yangu wakati wa kula,” anasema Dk Bisimba.

Anaongeza kuwa, hivi sasa anatumia magongo mawili kutoka sehemu moja hadi nyingine. Ameshauriwa kwa sasa kufanya hivyo wakati huu na daktari wake kulingana na hali yake ya kiafya.

Hata hivyo, Dk Bisimba anasema daktari wake amemwambia kuwa miezi kadhaa ijayo atarudi katika hali yake ya kawaida na kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

“Operesheni niliyofanyiwa ni kubwa. Kwa hiyo nimeambiwa nisiwe na haraka ya kukanyaga chini. Badala yake ninatumia magongo katika kipindi hiki,” anasema Dk Bisimba.

Anasema licha ya kuwa yupo kitandani bado anatoa msaada kwa njia ya simu kwa watu mbalimbali wenye matatizo ya kisheria huku wengine akiwaelekeza katika ofisi za LHRC, iliyoko Kijitonyama.

Anaamini kwamba sala za Watanzania ndizo zimemuwezesha kuimarika kiafya. Hivyo akawaomba wazidi kumuombea kwa sala.

Anasema ukilinganisha na hali ilivyo kuwa awali baada ya kutoka India, hali yake imekuwa bora zaidi na amekuwa mazoezi mepesi ya mara kwa mara ili kuvifanya viungo vyake kuimarika.

Anasema moja ya mambo ambayo amekuwa akitamani ni kupona na kuendelea na harakati zake za kuisaidia jamii kwa mambo mbalimbali hususan ya kisheria na haki.

Aelezea ajali ilivyotokea
Akisimulia ilivyokuwa siku ya ajali, Dk Bisimba anasema, “Hadi sasa siamini kilichotokea, kwa sababu nakumbuka siku ile barabarani hakukuwa na magari mengi na tulipofika eneo la mataa tulisimama na taa ya kijani ilivyowaka tuliondoka.

“Baada ya taa za kijani kuwaka na sisi kuondoka, ghafla nilisikia mshindo mkubwa na baadaye sikujua nini kilichoendelea, nafikiri nilipoteza fahamu. Nilirejewa na fahamu wakati nikajikuta hospitali na watu wakisema chana nguo yake. Ghafla nikajikuta napiga kelele; ‘Mama! Nguo yangu inachanwa,” alisema Dk Bisimba akisimulia jinsi hali ilivyokuwa mara baada ya kupata fahamu.

Akiwa hospitali, anasema ndiyo akawa anahadithiwa kuwa kuna vijana wawili waliosababisha tukio hilo.

Akaambiwa walifika katika gari lao na kuvunja kioo na kumtoa mtoto mjukuu wake na watu wengine.

Anasema baadaye, alifika mtu mmoja ambaye alijitambulisha kuwa ni baba wa vijana wawili waliosababisha ajali hiyo.

Dk Bisimba anasema vijana hao wote wawili walikamatwa na kufikishwa mahakamani, hata hivyo walikana kutenda kosa hilo na kesi yao imepangwa kusikiliza tena Februari 18, mwaka huu.

Dk Bisimba anasema: “Kusema kweli ile ilikuwa ni ajali haswa, kwa sababu barabara ile ni kubwa na hadi sasa sielewi gari lililotugonga lilitokea wapi.”

Anasema ameonyeshwa picha za jinsi gari ilivyoharibika, akaduwaa, maana kwa jinsi ilivyoharibika ni vigumu kuamini kama kuna mtu alipona.

Hata hivyo, anasema ni miujiza ya Mungu tu imewafanya wapone.


Safari ya India
Dk Bisimba anasema hospitali za Aga Khan na Moi, zilimsaidia kwa kiasi kikubwa kumpa matibabu, hivyo hana budi kushukuru.

Anasema baada ya kupewa ya rufaa ya kwenda India, haikuwa kazi rahisi kwake kutokana na maumivu makali aliyokuwa akiyapata akiwa safarini.

“Nilipanda ndege na kukaa eneo la kawaida kumbe nilihitaji ndege yenye kitanda nilale ili niweze kunyoosha mguu wangu. Hali hii ilinilazimu nikae huku nikiwa nimenyoosha mguu kwa sababu sikuruhusiwa kuukunja kutokana na chuma kilichokuwa nimewekewa ndani yake,” alisema Dk Bisimba.

Anabainisha kuwa, alipofika India alipelekwa moja kwa moja katika Hospitali ya Bhatal na kuwekewa ya oksijeni kutokana na umbali mrefu wa safari.

Anasema madaktari pia, walimuongezea damu chupa nne kwa ajili ya kumfanyia operesheni ikiwamo kumtoa chuma alichowekewa na kumwekea kifaa kingine cha kumsaidia.

“Sasa hivi namshukuru Mungu. Maana hata wakati narudi nikiwa katika ndege niliweza kukunja mguu wangu tofauti nilipokuwa ninaenda,” alisema Dk Bisimba
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top