Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, amemtumia
salamu za pole Mke wa Waziri Mkuu Mstaafu Mama Tunu Pinda aliyepatwa na
ajali ya gari, iliyotokea jana tarehe 08 Februai, 2016 akiwa safarini
kutoka Dodoma kwenda Dar es salaam.
Ajali
hiyo imetokea katika eneo la Mkundi lililopo katika Manispaa ya
Morogoro ambapo gari aliyokuwa akisafiria Mama Tunu Pinda, ilipinduka
baada ya kumgonga mwendesha pikipiki aliyeingia ghafla barabarani.
Katika
salamu hizo alizozituma kupitia kwa Waziri Mkuu Mstaafu Mheshimiwa
Mizengo Kayanza Peter Pinda, Rais Magufuli amesema amepokea kwa mshtuko
taarifa za kutokea kwa ajali hiyo na amemuombea Mama Pinda na Majeruhi
wengine kupona haraka.
"Kupitia
kwako Mheshimiwa Waziri Mkuu Pinda, naomba unifikishie pole nyingi kwa
mkeo Mama Pinda kwa kuumia katika ajali hii, na namuomba Mwenyezi Mungu
awaponye majeruhi wote ili waweze kuendelea na shughuli zao za kila
siku" alisema Rais Magufuli.
Mama Tunu Pinda anaendelea kupata matibabu Jijini Dar es salaam, na hali yake inaendelea vizuri.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dodoma
09 Februari, 2016
Post a Comment