ALIYEKUWA waziri katika serikali ya awamu ya kwanza hadi ya nne na Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kaskazini kwa miaka 35, Joseph Mungai.
Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto , Dk Hamis Kigwangalla akiwa na Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini, Cosato Chumi wakati wa ziara yake.
ALIYEKUWA waziri katika serikali ya awamu ya kwanza hadi ya nne na Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kaskazini kwa miaka 35, Joseph Mungai anadaiwa kurejesha serikalini eneo la hospitali ya wilaya ya Mufindi alilotuhumiwa kujipatia kinyemela na kulihodhi kwa muda mrefu bila kuliendeeleza.
Taarifa ya kurejeshwa kwa eneo hilo lililopo nyuma ya hospitali hiyo liyopo mjini Mafinga, wilayani humo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Jowika Kasunga kwa Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kya Tatu, Dk Hamis Kigwangalla alipotembelea hospitali hiyo juzi.
Akizungumzia mipaka ya kiwanja cha hospitali hiyo baada ya waziri huyo kutaka kujua kama haijakumbwa na uvamizi kutoka kwa wananchi, Kasunga alisema; “sehemu ya eneo la hospitali hii ilikuwa na mgogoro baada ya Mzee Mungai kudai kuimiliki kihalali.”
Alisema mgogoro huo ambao hata hivyo haukutajwa muda wake, umekwisha baada ya mbunge huyo mstaafu kurejesha eneo hilo mikononi mwa hospitali hiyo.
Akipokea taarifa hiyo, Dk Kingwala alitoa siku saba kwa uongozi wa halmashauri ya Mafinga Mji inayosimamia hospitali hiyo kujenga uzio utakaounganisha uzio wa hospitali hiyo ili kulinda mipaka yake.
“Pamoja na kujenga uzio nataka mniletee ofisini kwangu ramani ya eneo zima la hospitali na taarifa rasmi inayoonesha mgogoro baina yenu na mvamizi huyo umemalizika. Haya ni mambo ya kisheria, isije ikawa leo mnasema mgogoro umekwisha halafu kesho tukasikia mzee Mungai kaenda mahakamani,” alisema.
Dk Kigwangalla alizitaka halmashauri zote nchini kulinda maeneo yake kwa kuhakikisha yamesajiliwa na yana hati ili inapokuja mipango ya kuboresha au kutanua matumizi ya eneo kusiwepo na changamoto.
Akizungumzia huduma hospitali hapo, naibu waziri alisema; “hospitali hiyo ni muhimu katika eneo hilo lakini hamuipatii kipaumbele. Nimekagua na kujionea hospitali hii, kuna maeneo ya changamoto. Mfano ni vyumba vyake vya upasuaji, nyie mnaona kama mnavyo lakini kiukweli ni kama hamna kwani vilivyopo vinafanana na stoo ambacho sio kipimo chake,” alisema.
Alisema changamoto zingine katika vyumba hivyo ni uchakavu, havina mgawanyo wa vyumba, zinavuja, hazina maji, makabati yamechoka na paa lake halina viwango.
Alisema angetembelea hospitali hiyo kama mkaguzi angelazimika kufunga vyumba hivyo vya upasuaji visitumike kwasababu ya mapungufu yake.
Alitoa miezi mitatu kwa mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Mafinga, Shaibu Nnunduma kukamilisha ukarabati wa vyumba hivyo viwili vya upasuaji ili vikidhi vigezo vinavyotakiwa vinginevyo mkurugenzi huyo atatumbuliwa jipu.
Aliitaka hospitali hiyo pia kuanza mara moja ukusanyaji mapato yake kwa njia ya kielektoniki akisisitiza kwamba njia hiyo inapunguza mianya ya upotevu wa fedha zinazokusanywa.
Ili maagizo hayo yatekelezwe kwa ufanisi Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini, Cosato Chumi alimuomba waziri huyo kuangalia uwezekano wa wizara yake kuwasaidia kuboresha hospitali hiyo ambayo kwasasa inasimamiwa na halmashauri mpya ya Mafinga Mji badala ya halmashauri ya wilaya ya Mufindi.
“Mheshimiwa waziri halmashauri hii iliundwa Julai mwaka jana, imetokana na halmashauri ya Mufindi; bado haiko sawa kiutendaji na kimapato. Kwahiyo kuna mapato tunaitegemea mpaka sasa halmashauri mama ambayo wakati mwingine inatoa kama hisani tu,” alisema.
Akitoa mfano Chumi alisema zinaweza kuja Sh Milioni 17 kwa ajili ya sekta hiyo ya afya, lakini halmashauri yao pamoja na kubeba mzigo mkubwa wa kuhudumia hospitali hiyo ya wilaya inapata mgao wa Sh Milioni 3 tu.
Akiahidi kuyafanyia kazi maelekezo ya waziri huyo, mkurugenzi wa halmashauri hiyo alisema utekelezaji wake utanza mara moja wiki hii.
Post a Comment