Dereva wa lori lililobeba ng’ombe na kupata ajali juzi, Bakari Jafari (21), ameeleza namna safari yake ya kutokea Dodoma saa 11:00 jioni kuelekea mnada wa ng’ombe Pugu, ilivyoishia Tabata Matumbi saa 11:00 alfajiri.
Bakari ni miongoni mwa majeruhi sita waliolazwa Taasisi ya Mifupa Moi, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, wakiendelea kupatiwa matibabu baada ya kupata ajali iliyohusisha daladala yenye namba ya usajili T629 CRT aina ya DCM, lori la mchanga na gari alilokuwa akiendesha lenye namba za usajili T109 DDX na kuua watu wanne na wangine 25 kujeruhiwa.
Akisimulia mkasa huo jana, katika wodi ya majeruhi ghorofa ya kwanza iliyopo jengo jipya, Jafari alisema wakati ajali hiyo ikitokea aliiona na akajaribu kuikwepa bila ya mafanikio.
“Nilivyokuta ajali ilibidi nianze kuwakwepa, kweli nilijitahidi nikawakwepa, lakini ile DCM ilinivaa hivyo kugongana nayo uso kwa uso, ndipo nami nilipoteza fahamu,” alisimulia huku akipumua kwa tabu.
Jafari ambaye ameumia zaidi maeneo ya kichwani, kifuani na mkono wake wa kulia, alisema alibanwa na usukani wakati akijitaidi kukwepa ajali ile.
Alisema baada ya kupoteza fahamu alishtuka wakati ameshaokolewa na wasamaria wema ambao waliomtaka ataje namba za ndugu zake ili wapatiwe taarifa za ajali hiyo.
“Kweli kwa wakati ule nilikumbuka namba ya shangazi yangu, aliyeko mkoani Dodoma na dada yangu aishie Mbagala ambaye walimpigia na kuwaeleza taarifa hizo,” alisema.
Alisema pia abiria aliokuwa nao kwenye gari hakuwaona tena na wala hafahamu hali zao na mahali walipo hadi sasa.
“Kwenye gari tulikuwa wanne tumekaa mbele, ambao ni wenye zile ng’ombe waliokodi gari na wawili nyuma walikuwa wakiswaga ng’ombe ili wasichoke kabla ya kufika mnadani, lakini baada ya ajali sijui hata mmoja yuko wapi,” alisema.
Alisema baada ya hapo hakujitambua hadi alipojikuta yuko hospitali akipatiwa matibabu.
Alisema katika ajali hiyo alipoteza fedha zake kiasi cha Sh. 300,000 alizokuwa nazo mfukoni na simu yake ya mkononi.
HALI YAKE
Jafari akisimulia hali yake, alisema juzi hakuwa anajielewa kutokana na majeraha makubwa aliyokuwa nayo mwilini.
“Leo namshukuru Mungu naendelea vizuri, jana (juzi), sikuwa naweza kumtambua mtu yeyote, nilikuwa naona vivuli tu, lakini leo naweza kuongea japo kuwa nina maumivu makubwa sehemu ya kifua,” alisema.
Pia, alisema maeneo ya kifua ana maumivu makali yaliyotokana na kubanwa na usukani.
“Ashukuriwe Mungu, kila nikiwa naendesha gari huwa nalazimika kufunga mkanda na ndio sababu sikuumia maeneo ya chini ya miguuni na badala yake nilijibana tu maeneo ya kifua na usukani pamoja na kukatwa na vitu vyenye ncha kali kichwani na mkono wangu uliokuwa ukijitaidi kukwepa ajali ile,” alisema.
ASHUKURU MADAKTARI
Jafari ambaye wakati wote alikuwa akimshukuru Mungu kwa kumponya bila ya kujali maumivu aliyokuwa nayo, aliwashukuru madaktari wa Hospitali ya Amana, waliompatia huduma ya kwanza kabla ya kumpelekwa Moi.
“Nawashukuru hawa madaktari wa Moi, sijui cha kuwalipa ila Mungu atawalipa, wamejitahidi kunisaidia sikuwa najiweza lakini hadi sasa naweza hata kuzungumza, nilikuwa na hali mbaya sana, naamini Mungu atawalipa,” alisema.
Alisema amekuwa akipatiwa huduma zote za matibabu bila ya usumbufu wa aina yoyote ile.
ATUPIA LAWAMA DALADALA.
Jafari alisema anauzoefu wa kuendesha magari tangu mwaka 2002 na kwamba alichokibaini madereva wa daladala wamekuwa chanzo kikubwa cha ajali za barabadari jijini hapa.
Alisema madereva hao wamekuwa watu wa kujiamini kupita kiasi na kutojali magari mengine yanayopita barabarani hata yale makubwa kama malori na mafuso.
“Madereva wa daladala wamekuwa hawaheshimu wa madereva wengine ambao ni watumiaji wa barabara na ndio sababu wamekuwa wakifanya vurugu njiani,” alisema.
Alisema katika safari zake za kikazi, amekuwa akitoka mkoani kuja jijini hapa salama, lakini akifika kuanzia maeneo ya Mlandizi huwa mwangalifu zaidi kutokana na vurugu za madereva wa daladala.
“Nikifika Mlandizi tu, lazima nianze kuwa mwangalifu maana madereva wa daladala hawaheshimu magari mengine na kujiona wao ndio wenye haraka na wanaostahili kutumia barabara peke yao,” alisema.
Naye Meneja Ustawi wa Jamii na Uhusiano wa Moi, Almas Juma, alisema kuwa wagonjwa wote sita walioko hospitalini hapo wanaendelea vizuri.
Alisema wagonjwa hao wana majeraha katika maeneo ya kichwani, miguuni na michubuko sehemu mbalimbali za mwili.
Aliwataja majeruhi hao kuwa ni Bakari Jafari mkazi wa Mbagala, Mfaume Said mkazi wa Chanika, Neema Kimario (Gongo la Mboto), Rose Omary (Kiteto), Shabani Ally (Ubungo) na Victoria Msangi wa tabata.
Kwa upande wake, Daktari Kiongozi wa Hospitali ya Amana, Stanley Binagi, alisema wagonjwa wote 20 waliopokelewa aliwaruhusu juzi jioni baada ya hali zao kuendelea vizuri.
“Ukiacha wagonjwa sita tuliowapeleka Muhimbili na wale waliopoteza maisha, wagonjwa wengine wote hali zao ziliendelea vizuri hivyo tukawaruhusu kurudi nyumbani,” alisema.
Juzi saa 11alfari, gari aina ya DCM lenye namba za usaji T629 CRT, lilipoteza muelekeo kutokana na mwendo kasi na kugongana na lori la mchanga lililokuwa kwenye mwendokasi na kusababisha basi hilo kuhamia upande wa pili wa barabara na kugongana na lori hilo lilokuwa limebeba ng’ombe na kusababisha vifo na majeruhi kwa abiria.
Bint Wa Zuma Atiwa Mbaroni Kwa Tuhuma Za Ugaidi
2 hours ago
Post a Comment