Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, jana iliahirisha kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi Jimbo la Kigoma Kusini, iliyofunguliwa na aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, David Kafulila wa NCCR-Mageuzi dhidi ya Hasna Mwilima wa CCM.
Kesi hiyo ambayo ilivuta umati mkubwa jana, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Kigoma, iliahirishwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Sharmillah Sarwatt, kutokana na Jaji Ferdinand Wambali, aliyetakiwa kuanza kusikiliza kesi hiyo jana kutofika.
Akiahirisha kesi hiyo, Sarwatt alisema Jaji Wambali yuko safarini ndiyo maana hakufika hivyo kuahirisha kesi hiyo hadi Jumatatu ijayo.
Katika kesi hiyo iliyofunguliwa Novemba, mwaka jana, Kafulila anawakilishwa na mawakili Profesa Abdallah Safari na Tundu Lisu, wakisaidiana na Daniel Rumenyela.
Kwa upande wake, Mwilima anawakilishwa na wakili Kennedy Fungamtama pamoja na mawakili wa serikali wanaomwakilisha Msimamizi wa Uchaguzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ambao pia ni walalamikiwa katika kesi hiyo.
Kafulila, katika kesi hiyo, anaiomba Mahakama imtangaze kuwa mshindi kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi kifungu mamba 112(c) kwa hoja kwamba yeye ndiye aliyepata kura nyingi kwa mujibu wa matokeo ya kila kituo kwenye fomu namba 21B na kwamba msimamizi wa uchaguzi alimtangaza Hasna Mwilima kinyume cha matokeo halisi.
Jana, Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Kigoma ilifurika viongozi na wanachama wa vyama mbalimbali vya siasa, hali ambayo ilisababisha kuwapo ulinzi mkali wa jeshi la polisi ambao walikuwa na mabomu na silaha za moto
Loading...
Post a Comment