Mkuu wa wilaya ya Njombe Sarah Dumba amefariki dunia jana jioni ya baada ya kuugua ghafla
Mkuu wa mkoa wa Njombe Dkt Rehema Nchimbi amethibitisha kutokea kwa msiba huo, na kueleza kuwa marehemu Sarah alifariki majira ya saa moja jioni katika hospitali ya Kibena mjini Njombe ambapo alipelekwa kwa ajili ya uangalizi wa kiafya.
Dkt Nchimbi amesema kuwa, haijafahamika nini kilichosababisha kifo hicho, lakini huenda ikawa ni "Mshituko" maana jana asubuhi aliwasili ofisini kama kawaida, na kuendelea na shughuli zake akiwa hana tatizo.
Ameendelea kueleza kuwa, akiwa ofisini kwake, alianza kusema kuwa anajisikia vibaya, na kuamua kugawa majukumu yake kwa watendaji wengine, lakini hali yake ilizidi kutia mashaka na ndipo akapelekwa hospitali.
Dkt Nchimbi amesema, akiwa hospitali hali ilibadilika ndani ya muda mfupi na kuanza kutapika, na ilipofika majira ya saa moja alifariki dunia.
"Nadhani inaweza kuwa ni tension maana tupo kwenye maandalizi ya kilele cha maadhimisho ya wiki ya maji, na yeye amekuwa akishughulika sana na maandalizi hayo ambayo kilele chake ni kesho, sasa leo amefika ofisini kama kawaida, lakini baadaye akasema hajisikii vizuri, baadhi ya kazi akatuma watu, baadaye alikwenda hospitali, lakini muda mfupi baada ya kufika hali ikabadilika, akatapika sana na hapo ndipo alipopoteza maisha"Amesema Dkt Nchimbi.
Mkuu huyo wa mkoa amesema mipango ya maziko itatangazwa baadaye leo, lakini kwa taarifa za awali alizonazo ni kwamba huenda akapelekwa nyumbani kwao ambapo ni Dar es salaam, ingawa kuna taarifa nyingine zinadai kuwa nyumbank kwao ni Morogoro.
Post a Comment