Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

ZANZIBAR NJIA PANDA

Vijana waliovalia sare za Jeshi la KMKM na wengine nguo za kiraia huku wakiwa wameficha nyuso zao walipokuwa wakifanya doria eneo la Michenzani baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi wa Zanziba (ZEC), Jecha Salim Jecha kutangaza matokeo ya urais katika Uchaguzi wa Marudio, mjini Unguja

Zanzibar/Dar. Mgombea urais wa CCM, Dk Ali Mohamed Shein ametangazwa mshindi wa urais wa Zanzibar, huku akiwa na changamoto ya namna ya kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Changamoto hiyo inatokana na taarifa kwamba Chama cha UPDP kimeshinda kiti cha uwakilishi Jimbo la Ziwani, Pemba hivyo kuwa katika nafasi ya pili kwa kuwa na mwakilishi.

Hata hivyo, utata umegubika matokeo huku kukiwa na madai kwamba yalikosewa. Katika matokeo hayo yaliyobandikwa kwenye mbao za matangazo Asaa Hamad wa UPDP alipata kura 221 dhidi ya Mohamed Ali Salim wa CUF 153 wakati mgombea wa CCM, Suleiman Ali alipata kura 121.

Matokeo hayo yanakifanya chama hicho kuwa na nafasi ya kutoa Makamu wa Kwanza wa Rais huku kikiwa hakina wafuasi wengi ikilinganishwa na CUF kilichojitoa katika uchaguzi huo wa marudio uliofanyika juzi.

Matokeo ya urais

Dk Shein alitangazwa mshindi kwa kura 299,982 sawa na asilimia 91.4 huku mpinzani wake, Hamad Rashid Mohamed wa ADC akipata kura 9,734 sawa na asilimia 3.0.

Akitangaza matokeo hayo jana, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha alisema Maalim Seif Sharif Hamad wa CUF alishika nafasi ya tatu kwa kupata kura 6,076 sawa na asilimia 1.9 licha ya kujitoa katika uchaguzi huo, huku mshindi wa nne akiwa ni Issa Mohamed Zonga wa Sau aliyepata kura 2,018 sawa na asilimia 0.6.

Jecha alisema CUF na vyama vingine vilivyotangaza kujitoa vya Sau, NRA, Jahazi Asilia, DP, Demokrasia Makini na Chaumma havikufuata taratibu za kisheria na hivyo wagombea wake kuhesabika ni halali katika uchaguzi wa marudio.

Njiapanda

Licha ya ushindi huo, Dk Shein bado yuko njiapanda kukidhi matakwa ya kikatiba. Anatakiwa kutumia Ibara ya 9 (3) ya Katiba ya Zanzibar ambayo inasema muundo wa SMZ utakuwa wa SUK na utendaji wa kazi zake utafanywa katika utaratibu utakaohakikisha kuendelezwa kwa umoja na lengo la kufikia demokrasia.

Hata hivyo, ili aweze kuunda SUK, Katiba inamtaka kushirikiana na chama kilichoshika nafasi ya pili kwa wingi wa viti vya uwakilishi wa majimbo au asilimia 10 ya kura za urais.

Akizungumzia utata huo, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud alisema kuwa wakati Katiba ya Zanzibar ilipofanyiwa marekebisho mwaka 2010 na kuingiza kipengele cha kuundwa kwa SUK, mazingira yaliyojitokeza hivi sasa hayakuzingatiwa.

Masoud alisema kama utaitafsiri vizuri Katiba katika Ibara ya 39(3) kinachoeleza kuwa iwapo chama kilichotokea nafasi ya pili katika matokeo ya kura ya Uchaguzi wa Rais kimepata chini ya asilimia 10 ya kura zote, basi nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais itapewa chama chochote cha upinzani kilichotokea cha pili kwa wingi wa viti vya majimbo katika Baraza la Wawakilishi “...utaona kuwa neno wingi wa viti halielezei ni viti vingapi. Ukikiangalia kipengele hicho katika Katiba iliyoandikwa kwa Kiingereza maana yake ni idadi ya viti na siyo wingi wa viti. Hivyo idadi ya viti inayohesabiwa ni pamoja na vile viti ilivyopata CCM na chama cha pili ni kile kilichopata hata kiti kimoja, mgombea wake anapaswa kuwa ndiye Makamu wa Kwanza wa Rais,” alisema Othman.

Wakili wa Mahakama Kuu Zanzibar, Mohammed Sijamini alisema kinachotokea sasa ni upungufu wa Katiba, kwa kuwa wakati mabadiliko yalipofanyika hayakuangalia mazingira kama yanayotokea sasa.

Alisema pamoja na upungufu huo, bado Rais hawezi kukwepa kuunda SUK na hivyo atatumia busara zake kumpata Makamu wa Kwanza wa Rais, lakini kwa nafasi za mawaziri atalazimika kutumia nafasi zake 10, kuteua wawakilishi kutoka chama cha upinzani anachokitaka na kuwapata mawaziri wa kuunda Serikali.

Aliyekuwa Rais wa Chama cha Wanasheria wa Zanzibar, Awadh Ali Said alisema Katiba inamtaka Rais baada ya kuapishwa ndani ya siku saba awe ameteua jina la Makamu wa Kwanza wa Rais kutoka chama kilichoshika nafasi ya pili.

Awadh ambaye alikuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa chini ya Jaji Joseph Warioba, alisema kwa mazingira ya sasa Katiba haina jibu kuhusu kuundwa kwa SUK na hakuna uwezekano wa kuendesha Serikali kwa kutumia busara kwa kuwa kila kifungu cha Katiba kinajitosheleza.

“Nashindwa kuona mbele, yaani sipati picha,” alisema Awadh na kuongeza kuwa kwa nafasi 10 za uwakilishi alizonazo Rais, Katiba inasema kuwa atakaowateua angalau wawili watoke upinzani. Uzoefu unaonyesha amekuwa akiteua wanane kutoka CCM na wawili kutoka upinzani na hao wanane aliowateua wote aliwapa uwaziri.

Alisema Rais akitumia nafasi zake 10 kuteua wapinzani na kuwapa uwaziri, hiyo haitakuwa SUK, kwa kuwa nafasi hizo huzitumia hata kuteua wasio na vyama ili wamsaidie kwenye Serikali.

Hata hivyo, Mwanasheria wa kujitegemea Ali Saleh alisema SUK imekufa na kwamba hiyo imetokana na nyimbo ambazo wana-CCM wamekuwa wakiziimba huko nyuma wakitaka kuiua.

Saleh ambaye pia ni mbunge wa Mji Mkongwe (CUF), alisema Serikali inachotakiwa ni kufanya mabadiliko ya Katiba ambayo ni lazima iitishe Kura ya Maoni.

“Serikali itaundwa lakini haitakuwa ya Umoja wa Kitaifa, watajaribu kuibadilisha Katiba lakini wakitaka kufanya hivyo lazima waende kwenye Kura ya Maoni na ni wazi kwamba kwa hali ilivyo hicho ndicho kifo cha SUK.

“Inasikitisha kuona kuwa tunarudi tena katika mfumo wa chama kimoja kwa sababu ndicho kitakachokuwa kimehodhi Baraza la Wawakilishi na pia kuhodhi Serikali,” alisema Saleh.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba alisema hatima ya SUK ipo mikononi mwa Rais wa Zanzibar.

Alisema Zanzibar sasa imerudi hatua tano nyuma na kuondoa lengo la kuundwa SUK.

“Serikali ya Umoja wa Kitaifa ilikuwa na lengo la kuwaunganisha Wazanzibari, kurejesha hali ya amani na utulivu na kuleta umoja lakini kama sasa kilichofanyika katika uchaguzi ni kuidanganya dunia.”

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo Bisimba alisema sasa CCM imefanikiwa kurudisha serikali moja.

“Hapo tena Serikali ya Umoja Kitaifa haipo na itabaki Serikali ya CCM pekee jambo ambalo halionyeshi ukomavu wa kisiasa.”

Dk Bisimba alisema licha ya Baraza la Wawakilishi kuwa na wajumbe wengi wa CCM bado hawawezi kubadili Katiba ya Zanzibar na kufuta SUK.

Mabalozi wasikitishwa

Katika taarifa yao kwa vyombo vya habari baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, mabalozi wa Ubelgiji, Canada, Denmark, Umoja wa Ulaya, Finland, Ufaransa, Ujerumani, Ireland, Italia, Uholanzi, Norway, Hispania, Sweden, Uswisi, Uingereza na Marekani wameeleza kusikitishwa kwao na kitendo cha ZEC kurudia uchaguzi bila kuwapo mazungumzo ya kupata suluhisho la kisiasa.

“Ili mchakato wa uchaguzi uwe unaokubalika ni lazima uwe na uwakilishi mpana wa matakwa ya wananchi.

“Tunatoa wito kwa Serikali ya Tanzania kuonyesha uongozi kuhusu suala la Zanzibar na kuanzisha mazungumzo ya vyama vya siasa kwa mtazamo wa kuhakikisha uwepo wa amani na umoja katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Tunawapongeza Wazanzibari kwa kuwa watulivu wakati uchaguzi wa marudio ulipofanyika na tunatoa wito kwa vyama vyote vya siasa na wafuasi wao kuanzisha upya mchakato wa kupatikana mwafaka wa kitaifa,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top