Wananchi waliozungumza na gazeti hili jana mjini Chake Chake walisema kuwa jambo hilo si siri, wamekuwa wakitangaziwa katika misikiti, mikusanyiko ya watu na katika mitaa yao kupitia kwa masheha kwamba wanatakiwa kulala mapema.
Mhudumu wa nyumba ya wageni mjini Chake Chake, Salum Ramadhan Ali aliliambia gazeti hili kuwa wameambiwa na masheha wawatangazie wanaokodi vyumba kuwa mwisho wa kurudi ni saa tatu usiku.
“Mpaka saa tatu usiku wanatakiwa kuwa vyumbani maana wanaweza kupatwa na jambo lolote. Pia, tunawaomba walipe kabisa pesa ya chumba ili wakikutwa na lolote wawe wameshatulipa,” alisema Ali.
Alisema mbali na kupewa maelekezo hayo ambayo hawana budi kuyatekeleza, idadi ya wateja katika nyumba za wageni imepungua kwa maelezo kuwa huenda watu wana hofu na uchaguzi huo wa marudio unaofanyika Jumapili.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwenye zaidi ya nyumba tatu za kulala wageni, umebaini kuwa tangazo hilo hutolewa kwa wageni wote wanaofika na hutahadharishwa kutotembea usiku.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Pemba, Mohammed Sheikhan hakupatikana kufafanua suala hilo na sababu ya watu kuwa na hofu kiasi hicho kutokana na simu yake ya mkononi kutokuwa hewani.
Post a Comment