Rais wa Jamuhuri ya Mungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli amekabidhi gari la kubebea wagonjwa kwa hosipitali ya wilaya ya Chalinze, Ikiwa ni utekelezaji wa ilani na ahadi ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi CCM kwa wananchi ikiwa ni pamoja na wa jimbo la Chalinze.
Gari hilo la kubebea wagonjwa limekabidhiwa kwa niaba ya Rais, na Katibu Mkuu Ikulu Peter Ilomo kwa Mbunge wa Jimbo la Chalinze Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete Ikulu jijini Dar es Salaam.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi gari hilo, Katibu Mkuu Ikulu Ndugu Peter Ilomo amesema gari hilo limetolewa na Mheshimiwa Rais kwa hosipitali hiyo ikiwa ni kuitikia wito na utekelezaji wa ilani na ahadi ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi CCM ya kuboresha huduma ya afya kwa wananchi wake kote nchini.
Aidha, Ndugu Ilomo amewaomba viongozi wa jimbo la Chalinze kulitumia gari hilo kwa matumizi yaliyokusudiwa ya kuwahudumia wananchi wa eneo hilo.
Akipokea gari hilo kwa niaba ya wananchi wa jimbo na Wilaya ya Chalinze, Mbunge wa jimbo la Chalinze Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete amemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa msaada huo na kuahidi kulitumia gari hilo kwa malengo yaliyokusudiwa, na kusema kuwa, utendaji kazi wa Rais Magufuli umekuwa ukiungwa mkono na wananchi wa kada mbalimbali na kuwaomba watanzania kuzidi kumuombea kwa Mungu.
Kwa upande wake Dakta Nasoro Ally Matuzya, amesema gari hilo limekuja kwa wakati muafaka kwa kuwa umezingatia utekelezaji wa malengo ya Milenia hususan lengo namba nne linalosisitiza kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano
Naye Mwenyekiti wa Halmshauri ya Wilaya ya Chalinze Ndugu Saidi Omar Zikatimu amesema gari hilo la kubebea wagonjwa litakuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa jimbo hilo la Chalinze hususan katika kusaidia kutoa wagonjwa ambao wako katika maeneo ya vijijini wilayani humo na kuwafikisha katika hospitali ya Chalinze na hivyo kunusuru maisha yao kwa kupata huduma za afya kwa haraka.
Mbali na Wilaya ya Chalinze kupata msaada wa gari hilo la kubebea wagonjwa, tayari magari mengine mawili ya kubebea wagonjwa yameshakabidhiwa katika vituo vya afya vya Kiroka na Kisemu mkoani Morogoro.
Hospitali mpya ya Wilaya ya Chalinze imepanda hadhi kutoka kituo cha Msoga ambayo ilikuwa haina gari la kubebea wagonjwa na hivyo kufanya usafirishaji wa wagonjwa kutoka hospitali hiyo hadi hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Pwani ya Tumbi au kutoka maeneo ya vijijini kuwa mgumu.
Imetolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu
18 Machi 2016.
Post a Comment