Makamba pia amemshauri Lowassa kuachana na harakati za kuwania urais kwa kuwa ni muda mrefu tangu alipogombea kwa mara ya kwanza mwaka 1995 na kuishia kwenye uteuzi ndani ya CCM.
“Kuondoka kwa Lowassa kwenda upinzani ndiyo kulirahisisha sisi (CCM) kushinda uchaguzi kwa sababu kuliwaondolea wapinzani hoja mbili muhimu ambazo ni ufisadi na mabadiliko,” alisema Makamba, ambaye alikuwa msemaji wa kampeni za CCM kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita, wakati wa mahojiano na Mwananchi ofisini kwake Jumapili.
Lowassa, ambaye alikuwa waziri mkuu wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne kabla ya kujiuzulu mwaka 2008 baada ya kuibuka kashfa ya Richmond, alijiengua CCM Julai 28, mwaka jana ikiwa ni siku chache baada ya jina lake kuchujwa pamoja na wagombea wengine 33 wa urais kwa tiketi ya CCM.
“Niliwekewa mizengwe kuhakikisha jina langu halifiki Kamati Kuu na Halmashauri Kuu,” alisema Lowassa wakati akitangaza kujiengua CCM na baadaye akajitetea kuwa kuhusishwa kwake kwenye sakala la Richmond kulitokana na kupokea maagizo kutoka juu.
Akiwa Chadema, Lowassa alipitishwa kugombea urais na akaungwa mkono na vyama vingine vitatu vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), hali iliyomfanya aweke rekodi ya upinzani tangu kurejeshwa kwa vyama vingi baada ya kuzoa asilimia 39.97 za kura akizidiwa na John Magufuli wa CCM, ambaye alipata asilimia 58.4.
Katika mazungumzo na Mwananchi, Makamba alikiri CCM kupata ushindani mkubwa kutoka vyama vya upinzani katika uchaguzi huo uliokuwa na msisimko, lakini akasema kuhama kwa Lowassa kuliwapa nguvu zaidi.
“Kuhusu Lowassa kujiunga na upinzani kwamba ndio kuliwapa nguvu (Ukawa), hapana. Suala hili kwangu nalitazama tofauti,” alisema Makamba.
“Mnapomchukua mtu (Lowassa) ambaye miaka 10 iliyopita mmekuwa ndiyo mnashika picha yake kwamba ni kielelezo cha rushwa na ufisadi ndani ya nchi na CCM, halafu mnamchukua, mnaenda naye kwenye kampeni maana yake ile hoja (ya ufisadi) mmeamua kuiachia.”
Makamba pia alisema Lowassa amekuwa sehemu ya mfumo wa utawala na uongozi wa nchi kwa miaka 40, hivyo hawezi kuwa kinara wa mabadiliko.
Alisema kitendo cha Chadema kuhubiri mabadiliko huku mgombea akiwa Lowassa, maana yake ni kwamba wameamua kuiacha hoja hiyo.
“Kwa tathmini yangu na utafiti tulioufanya, hizo hoja mbili ambazo siku zote zilikuwa silaha za upinzani, wameamua kuziachia na matokeo yake ilikuwa rahisi kwetu (CCM) kupata ushindi,” alisema.
Alipoulizwa atamwabia Lowassa nini siku wakikutaka, Makamba alisema: “Kwanza, nimemsikia akisema atagombea tena mwaka 2020, nitamwambia mambo mawili; hii habari kuwa aliibiwa kura aachane nayo maana si kweli, pia inampunguzia heshima maana uchaguzi umeisha na wananchi wameridhika lakini wewe peke yako unabaki kualalamika.”
Pili, alisema hoja ya pili itakuwa ni kumshauri asigombee urais mwaka 2020 kwa kuwa CCM watamshinda na atakuwa ametumia miaka 25 kuwania nafasi hiyo bila mafanikio.
“Alianza kuutaka urais mwaka 1995 ni kipindi kirefu na mle bungeni tutakuwa na wabunge ambao kabla hawajazaliwa, Lowassa alikuwa anagombea. Nadhani nchi hii watu wana vipaji, waachiwe nafasi watoe mchango wao kwenye kujenga demokrasia ya nchi yetu. Kifupi apumzike,” alisema Makamba.
Katika uchaguzi wa mwaka 1995, Lowassa aliondolewa mapema kwenye mbio za urais kwa tiketi ya CCM na mwaka 2005 hakuchukua fomu, badala yake akawa nguzo kuu ya kampeni za rafiki yake, Jakaya Kikwete ambaye aliibuka kidedea CCM na baadaye kushinda urais. Baada ya uchaguzi, Kikwete alimteua Lowassa kuwa Waziri Mkuu.
Akizungumza na wazee wa Chadema jimbo la Ubungo hivi karibuni, Lowassa aliwataka kutokata tamaa na kujipanga kimkakati kujiandaa na kuimarisha chama kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka 2020 na kuahidi kugombea tena.
Nguvu ya upinzani
Makamba pia alisema alitegemea nguvu ya upinzani kuongezeka kadri muda unavyokwenda kwa sababu baada ya zaidi ya miaka 23 tangu kurejeshwa kwa mfumo wa siasa za ushindani, upinzani usingeendelea kubakia uleule.
Alisema hivi sasa mwamko wa Watanzania katika kusikiliza mawazo na fikra tofauti umeongezeka na kwamba CCM imepewa changamoto kutokana na mabadiliko ya mfumo katika jamii, uhuru wa habari, wa kuamua na kujieleza.
“Yaliyotokea ni matokeo ya mafaniko ya maendeleo ya demokrasia katika nchi yetu miaka 10 iliyopita,” alisema.
Alisema hali hiyo imewafanya wananchi kutoogopa kujitokeza na kuunga mkono waziwazi upinzani, akivituhumu baadhi ya vyombo vya habari kujipambanua msimamo wake kwa wagombea wa upinzani.
Wanaomponda Rais Magufuli
Kwa nyakati tofauti viongozi wa Chadema, wakiongozowa na mwenyekiti wao Freeman Mbowe wamenukuliwa wakisema kuwa mambo yanayofanywa na Rais Magufuli ni mawazo ya wapinzani na yapo katika ilani ya uchaguzi ya Chadema, lakini Makamba amepinga akisema wanamsifia Rais ‘kwa mamna yake’.
“Nadhani wanajaribu kudandia treni inayokwenda vizuri. Pengine ndiyo namna nzuri ya kiungwana ya kumsifia mtu kwa sababu wamekosa ujasiri wa kusema anafanya kazi nzuri,” alisema Makamba.
“Ilani yetu ukiisoma ina vipaumbele vikubwa vinne; cha kwanza ni kupinga rushwa, uzembe na ubadhilifu wa mali ya umma. Hatua zinazochukuliwa sasa ni ahadi tulizotoa katika ilani. Pili, wakati wa kampeni Rais Magufuli aliahidi haya anayofanya. Tulitegemea atayafanya kwa sababu aliyasema katika kampeni.”
Alisema CCM ilimteua Magufuli kwa sababu ilijua inateua aina ya kiongozi atakayesaidia kutokana na kujulikana kwa utendaji wake.
“Hiyo ilani ya Chadema sisi hatuijui na hata mgombea wao alikuwa anaongea dakika tatu, sasa kwa muda huo ataongea jambo gani la kuigwa,” alisema Makamba huku akieleza mambo mengine mawili yaliyokuwepo kwenye ilani ya CCM kuwa ni ajira na umasikini.
Post a Comment