Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ilala wamepewa mpaka tarehe 24 Machi mwaka huu wawe wamekwenda kuhakikiwa katika ofisi za utawala za Halmashauri hiyo katika kutekeleza agizo la Mhe.Rais Dkt John Pombe Magufuli la kuhakiki watumishi wote wa umma.
Akizungumza kwa njia ya simu ofisini kwake msemaji wa Halmashauri ya Ilala Bi. Tabu Shahibu amesema tangazo limeshatoka na watumishi wote wanatakiwa kufika kuhakikiwa katika ofisi za utawala ambapo wanatakiwa kwenda na nyaraka mbalimbali muhimu zizohusu ajira zao.
Bi Tabu Shahibu amezitaja nyaraka hizo ambazo mtumishi anatakiwa kuambatanisha wakati wa uhakiki wake kuwa ni vyeti halisi vya taaluma,barua ya kuajiriwa na kudhibitishwa kazini, salary slip na picha ndogo za hivi karibuni.
“Zoezi la uhakiki linaendelea vizuri na watumishi wengi wamejitokeza kwa wingi na tunategemea kumaliza zoezi hili March 24 mwaka huu ili kuandaa taarifa rasmi ya kujua watumishi halali na wale watumishi hewa” Alisema Bi Tabu.
Aidha Bi Tabu Shaibu amesema kumekuwa na changamoto ya watumishi wengi kutokuwepo kwenye vituo vya kazi ikiwa wengine wapo masomoni na likizo ila wameshatoa taarifa ya kuwaita ili kufanyiwa uhakiki mara moja ili kuendana na muda uliotolewa na Mhe Rais Magufuli wa siku 15.
Zoezi la uhakiki wa watumishi wa umma katika limekuja mara baada ya uchunguzi uliofanywa katika mikoa ya Singida na Dodoma katika Halmashauri 14 na kugunduwa wafanyakazi hewa 202 wanaolipwa mishahara na hivyo Mhe. Rais Magufuli kutoa agizo la kuhakiki watumishi wote katika Wizara,mikoa,Wilaya,Idara, Taasisi na Wakala za Serikali ndani ya siku 15.
MWISHO
Post a Comment