SIKU moja tu baada ya kuhojiwa na Polisi kwa saa tatu visiwani hapa, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, amesema njia pekee ya kumwondoa Rais Dk. Ali Mohamed Shein madarakani, ni kuendeleza mgomo baridi.
Maalim Seif alisema hayo jana alipozungumza na wafuasi wa chama hicho, Kilimahewa Wilaya ya Mjini Unguja, katika ziara zake za kuimarisha CUF katika kila wilaya za Zanzibar.
Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, Salum Msangi, aliwaambia waandishi wa habari juzi kuwa jeshi lake lilimhoji Maalim Seif kwa saa tatu.
Ingawa Msangi hakusema walimhoji katika masuala gani, Wakili wa Maalim Seif, Awadh Ali Said, alisema juzi kuwa mteja wake aliwekwa kati na maafisa 12 wa polisi, ambao walitaka kujua pamoja na mambo mengine, ni kwa nini hawakatazi wafuasi wake kumwita Rais.
Akizungumza jana, Maalim Seif alisema mataifa ya nje hayawezi kumwondoa Dk. Shein madarani lakini kama wananchi na wafuasi wa CUF wataungana kufanya mgomo baridi, haitafika miezi mitatu kabla hajaachia madarakara.
“Wala msidhani kwamba atakuja Mmarekani kumwondoa Dk. Sheni,"alisema Maalim Seif na kuongeza kuwa: "Hii ni nchi, taifa lingine haliwezi kuingilia."
Katibu mkuu huyo alisema anachoweza kufanya Mmarekani ni kuzuia misaada na wameshalianza hilo.
"Sasa hawa wezetu mataifa ya nje wanatubeba na anayebebwa hujikaza. Tukikaza uzi huyu bwana miezi mitatu hafiki kwa sababu hana fedha, ataweza vipi kuiongoza Serikali wakati baadhi ya mataifa yameshazuia misaada yao?" alihoji.
CUF imegoma kuitambua serikali ya Dk. Shein kwa madai kuwa uchaguzi mkuu wa marudio wa Machi 20, mwaka huu, uliomwingiza madarakani ni batili.
CUF inadai kutambuliwa kwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana, ambao ilielekea kushinda na ambao matokeo yake yalifutwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanizbar (ZEC), Jecha Salum Jecha, kwa madai ya kuwapo kwa kasoro nyingi.
ZEC ilifuta matokeo hayo licha ya waangalizi wa ndani na wa kimataifa, wakiwemo kutoka Jumuiya ya Madola, Jumuiya ya Ulaya (EU) na Marekani kuutangaza kuwa huru na haki.
Akizungumza katika kikao hicho jana, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Nassor Ahmed Mazrui, alisema Maalim Seif ndiye mkombozi wa Wazanzibari kama alivyokuwa Nelson Mandela wa Afrika Kusini.
Alisema wana imani kuwa Maalim Seif ndiye Rais wa Zanzibar na wataendelea kumwita Rais na hakuna wa kuwazuia kwa sababu yeye ndiye aliyeshinda katika uchaguzi wa Oktoba 25.
Alisema kitendo cha wafuasi wa CUF kuwatenga wafuasi wa CCM na viongozi wa Serikali walioko madarakani ni halali na kuwataka wafuasi hao kuendelea na mgomo huo.
“Hakuna cha kuogopa, endeleeni kuwagomea," alisema Mazrui na kuwataka wasiende katika shughuli zao, mazishi na wanaouza maduka wasiwauzie bidhaa mpaka haki yao irejee.
Post a Comment