Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli amesema kuwa baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma walioondolewa chuoni hivi karibuni hawakuwa na sifa za kujiunga na masomo chuoni hapo.
Akizungumza leo katika uzinduzi wa Maktaba mpya ya Kisasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Rais Magufuli amewataka watanzania kuweka siasa kando nakuzungumzia masuala ya msingi, huku akiwashangaa wanasiasa waliojitokeza kuwatetea wanafunzi hao.
“Nimeshukuru wale vijana wameondoka. Wanasiasa haohao, ‘eti ooh.. hao vijana wamekosa pa kulala.. it’s nonsense’. Taifa letu tuliweke mbele kwanza. Siasa zije nyuma,”alisema.
Alisema kuwa baadhi ya wanafunzi ambao walibainika kuwa na elimu ya kidato cha nne waliofeli masomo yao na kuruhusiwa kuendelea na masomo ya elimu ya juu ni watoto wa viongozi.
“Ukimchukua mtoto wa form four ukampeleka pale, hata kama atafanikiwa kupata degree… itakuwa ya ajabu. Na baadhi ya watoto waliopelekwa pale ni watoto wa viongozi. Watoto wa Maskini wenye qualification wamekosa nafasi za kwenda Chuo Kikuu. Watoto wa watu fulani fulani wanapelekwa wakati walifeli. It can’t be,” Dk. Magufuli alisisitiza.
Rais Magufuli aliongeza kuwa Serikali yake haitaruhusu fedha zinazopaswa kutumika kwa ajili ya maendeleo ya wananchi kupelekwa kwa ‘vilaza’ huku waliofaulu wakikosa mikopo ya elimu ya juu.
Dk. Magufuli ameahidi kuwa Serikali yake itahakikisha wanafunzi waliofaulu kwa kiwango cha daraja la kwanza na la pili (division 1 &2) wanajengewa mazingira mazuri ya kuendelea na masomo.
“Waliofeli watafute vyuo vyenye size yao,” alisisitiza.
Post a Comment