Mbunge wa Momba (CHADEMA), David Silinde akizungumza na waandishi wa habari kuelezea msimamo wa kambi rasmi ya upinzani bungeni kuhusu bajeti kuu ya Serikali ya mwaka 2016/17. Katikati ni Mbunge wa Vunjo, James Mbatia na Mbunge wa Viti Maalum (CUF), Riziki Mngwali.
Mbunge wa Vunjo (NCCR- Mageuzi), James Mbatia akizungumza na waandishi wa habari kuelezea msimamo wa kambi rasmi ya upinzani bungeni kuhusu bajeti kuu ya Serikali ya mwaka 2016/17. Kushoto ni Mbunge wa Momba (CHADEMA), David Silinde na Mbunge wa Viti Maalum (CUF), Riziki Mngwali.(PICHA NA ISMAIL NGAYONGA- MAELEZO)
Na Jonas Kamaleki-MaelezoDodoma
KAMBI rasmi ya Upinzani Bungeni imemuunga mkono Rais, Dkt. John Pombe Magufuli katika juhudi zake za kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na kuelekeza fedha hizo katika miradi ya maendeleo na huduma za jamii kama ujenzi wa miundombinu ya barabara na reli.
Pongezi hizo zimetolewa leo mjini Dodoma na Mbunge wa Momba (CHADEMA), David Silinde wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu bajeti kuu ya Serikali ya mwaka 2016/17.
“Tunamuunga mkono Mhe. Rais John Pombe Magufuli kwa kuondoa posho za vikao (Sitting Allowances) na tunamwomba aondoe posho hizo kwa wabunge nao watumie mishahara yao ili kuwe na usawa,” alisema Silinde.
Silinde alisema kuwa Kambi Rasmi ya Upinzani inaunga mkono juhudi za Mhe Rais Magufuli za kukusanya kodi ambayo inabidi ielekezwe kwenye miradi ya maendeleo na huduma za kijamii.
“Tunaungana na Serikali kukata kodi kwenye kiinua mgongo cha wabunge lakini tunamuomba Mheshimiwa Rais apanue wigo wa kodi hiyo hadi kwa wakuu wa Mikoa na Wilaya,” alisema Silinde.
Kwa upande wake, mbunge wa Jimbo la Vunjo (NCCR-Mageuzi), Mhe. James Mbatia amesema kuwa Kambi Rasmi ya Upinzani inamuomba Mhe. Rais Magufuli kufuta posho za vikao kwa wabunge haraka ili kuleta usawa kwa watanzania wote.
Post a Comment