Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amewachokoza tena wabunge baada ya kuitaka Serikali kuanza kukata kodi katika posho za wawakilishi hao ili kuongeza wigo wa mapato.
Zitto amesema hatua ya Serikali kuondoa msamaha wa kodi katika malipo ya kiinua mgongo cha wabunge katika bajeti ya Serikali ya 2016/17 ni jambo jema lakini isiishie hapo kwa kuwa viongozi hao bado wana mapato mengi yasiyokatwa kodi yakiwemo ya posho.
Kauli ya mbunge huyo wa Kigoma Mjini ni mwendelezo wa msimamo wake wa kupinga wabunge kulipwa posho ya vikao bungeni na katika Bunge la 10 alipokuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema) aliongoza kampeni ya kupinga ongezeko la posho hiyo bila mafanikio.
Aidha, pendekezo lake kutaka posho za wabunge zikatwe kodi limekuja siku mbili tangu Naibu Spika, Dk Tulia Ackson atangaze kukata posho za wabunge watakaokuwa wakisaini kuingia bungeni na baadaye kuondoka na waathirika wa kwanza wa hatua hiyo watakuwa wapinzani wanaosusia vikao vyake.
Akitoa maoni katika mchaparo wa uchambuzi wa Bajeti ya Serikali ya mwaka 2016/17 ulioandaliwa na Kampuni ya Ukaguzi wa Hesabu ya KPMG juzi usiku, Zitto alisema kiinua mgongo hicho kilichoanza kutolewa mwaka 2010 kimekuwa kikitolewa bila kufuata sheria.
Alisema mwaka 2010 pensheni hiyo iliongezwa mara mbili kinyume na sheria na mwaka jana fedha hizo ziliongezwa tena takriban mara nne zaidi bila kukatwa kodi.
Zitto alisema wanashangaa kwa nini kodi ya kiinua mgongo imeanzishwa mwaka huu wakati wabunge watalipwa mwaka 2020.
“Nilichokuwa na natarajia ni kuanzisha kodi kwenye posho. Sisi (wabunge) tuna posho za aina nyingi na kubwa zaidi ni ile posho ya kikao ya Sh220,000 kwa siku,” alisema.
“Hii posho haikatwi kodi na wala siyo fedha za kujikimu (per diem) ambayo unapewa kwa ajili ya chakula na malazi.”
Alisema kwa mwaka mbunge anapata takriban Sh40 milioni za posho (Sh200 milioni kwa miaka mitano) wakati kiinua mgongo ni takriban Sh172 milioni baada ya miaka mitano hivyo posho zingeweza kuingiza mapato mengi zaidi.
Katika uchambuzi wa bajeti hiyo, Mkurugenzi wa kodi na huduma wa kampuni wa KPMG, David Gachewa alisema uanzishwaji wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika sekta ya benki utawaumiza wananchi lakini hakukuwa na namna nyingine zaidi ya Serikali kuianzisha ili kuongeza wigo wa mapato.
Hata hivyo, alisema anaona utata katika utekelezaji wa ukusanyaji mapato hayo iwapo Serikali itatoa mashine za kielektroniki za kutolea risiti (EFD) kwa benki hizo au Kamishna Mkuu wa TRA atawaandikia barua kutozitumia mashine hizo kama Serikali ilivyompa madaraka hayo katika bajeti.
“Hii siyo mara ya kwanza kuwapo ugumu katika utekelezaji wa baadhi ya hatua za ukusanyaji mapato. Naamini Chama cha Benki Tanzania (TBA) kitakaa na Serikali kuona ni namna gani watalitatua tatizo hilo,” alisema Gachewa.
Kuhusu hatua ya Serikali kuzitaka taasisi zote za umma kutumia huduma za bima za Shirika la Bima la Taifa (NIC), Gachewa alisema si kitu kizuri kwa sababu kitafanya Serikali ianze kushindana na sekta binafsi.
“Kuna dalili za wazi kuwa Serikali inafanya biashara jambo ambalo halikutarajiwa. Serikali ilitakiwa iache sekta ya bima mikononi mwa sekta binafsi na yenyewe iweke mazingira wezeshi,” alisema.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Kitila Mkumbo alisema hatua nyingi zilizochukuliwa katika uandaaji wa bajeti hizo zimekosa ushahidi kama zitatekelezeka ipasavyo.
Mtaalamu huyo wa masuala ya elimu na saikolojia alisema uamuzi wa kupunguza safari za nje una matatizo sababu unaifanya Tanzania kutokuwa na muunganiko na ulimwengu na kitendo cha bajeti hii kubana zaidi matumizi kitaifanya nchi ishushe hadhi yake kimataifa.
“Jambo la msingi katika udhibiti wa safari za nje lingekuwa kupunguza posho za maofisa wanaosafiri nje ya nchi na siyo kupiga marufuku mpaka kwa kibali maalum,” alisema.
Kuhusu bajeti ya elimu, Profesa Kitila alisema iwapo fedha zote Sh4.4 trilioni zilizopangwa zitatolewa ni jambo jema katika sekta hiyo muhimu katika maendeleo.
Hata hivyo, alionya kuwa historia inaonyesha bado hazitaleta matokeo mazuri kwa kuwa sehemu kubwa huelekezwa katika kulipa mishahara na kuimarisha miundombinu badala ya kugharamia programu za kuongeza ubora wa taaluma.
Wadau wengi waliipongeza Serikali kutenga asilimia 40 ya bajeti katika miradi ya maendeleo ila walionyesha hofu kuwa sehemu kubwa ya kodi inategemea sekta binafsi jambo linaloweka ugumu katika mazingira ya ufanyaji biashara.
Profesa wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Honest Ngowi alisema takriban asilimia 51 ya mapato ya bajeti hiyo iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango inagusa sekta binafsi na kuhoji kama kutakuwa na ukuaji mzuri wa sekta hiyo.
“Uamuzi wa kuanzisha VAT katika utalii haukuwa mzuri badala yake Serikali ilitakiwa ivutie watalii wengi ili ipate kodi katika maeneo mengine ya tozo kutokana na idadi kubwa,”alisema na kuongeza: “Kodi inatakiwa kuwa chombo cha mapato na msingi mkubwa wa maendeleo.”
Post a Comment