Ofisi ya Rais Ikulu imewanyima vibali vya kusafiri kwenda Marekani wabunge wawili wa Kambi ya Upinzani, bungeni na kumruhusu mbunge wa Geita Mjini (CCM), John Kanyasu.
Wabunge hao wa kambi ya upinzani waliochaguliwa kwenda Marekani ni Savelina Mwijage (CUF) na Mwita Mwaikabwe (Chadema)
Wabunge hao watatu ni wajumbe wa Kamati ya Masuala ya Ukimwi, lakini baada ya kunyimwa vibali hivyo wamejitoa kwenye kamati hiyo wakipinga kitendo hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari bungeni mjini Dodoma, mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Mwikwabe alisema walipata barua ya kuteuliwa kushiriki safari hiyo kutoka Ofisi ya Bunge Mei 24.
“Tunapenda kukufahamisha kuwa Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amekuteua kushiriki mkutano wa ngazi ya juu ya maamuzi kuhusu Ukimwi duniani utakaofanyika 08-10 New York, Marekani,” alinukuu barua hiyo iliyosainiwa na Patson Sobha kwa niaba ya Katibu wa Bunge.
Katika barua hiyo wametajwa wabunge wengine kwenye safari hiyo kuwa ni mbunge wa viti maalum (CUF), Savelina Mwijage.
“Nikiwa Tarime nilipata simu kutoka kwa Patson kwamba, Naibu Spika alipokea simu kutoka Ikulu kuwa imezuia vibali vyetu vya kwenda Marekani na badala yake Kanyasu ameteuliwa,” alisema Mwikabe.
“Tunashangaa, kuteuliwa tuliambiwa kwa barua, lakini kukataliwa tuliambiwa kwa simu,” alisema Mwita.
Alisema kutokana na kutopewa kibali, wajumbe wote wa kambi hiyo wamejitoa kwenye Kamati ya Bunge ya Ukimwi.
“Hayo yote yanafanyika kwa sababu Naibu Spika hatupendi kabisa wabunge wa upinzani ndiyo maana wametufanyia haya,” alisema.
Kwa upande wake, mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi), James Mbatia alisema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwaambia katika mkutano wa wabunge wote kuwa hawahusiki katika uombaji wa vibali kutoka Ikulu.
“Mimi mwenyewe nimeshawahi kusafiri zaidi ya mara tatu mbona sijawahi kuomba kibali kutoka Ikulu?”alihoji Mbatia.
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alihoji kama wabunge hao ndiyo wenye haki ya kusafiri. Pia alihoji haraka waliyonayo wabunge hao wakati walishapeleka malalamiko yao kwa maandishi dhidi ya Naibu Spika, Dk Tulia Ackson.
“Kwani wanaharaka gani wao? Si walishapeleka malalamiko hayo na yapo kwenye kamati. Wasubiri uamuzi ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge),” alisema.
Post a Comment