Rais Dkt. John Pombe Magufuli akipokea Taarifa ya Mwaka ya utendaji wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo Kamishna Valentino Mlowola Ikulu jijini Dar es Salaam April 11,2016.Picha na Ikulu.
****
Hussein Makame-Maelezo
Jumla ya washitakiwa 572 wamepatikana na hatia kufuatia tuhuma za rushwa zilizowakabili katika mahakama mbalimbali nchini katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2015.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Kamishna Valentino Mlowola katika taarifa iliyotolewa kwa niaba yake na Afisa habari wa taasisi hiyo Mussa Misalaba.
Taarifa hiyo inaonesha kuongezeka kwa idadi ya washitakiwa waliopatikana na hatia ambapo mwaka 2010 washitakiwa 61 walitiwa hatiani wakati hadi kufikia Desemba 2015 mahakama iliwatia hatiani washitakiwa 188.
Alisema katika mwaka 2015 (Januari-Desemba) jumla ya matukio ya rushwa 5,000 yaliripotiwa na aina ya rushwa iliyoripotiwa mara nyingi ni matumizi mabaya ya madaraka.
Taarifa hiyo inaonesha kuwa katika kipindi hicho cha miaka 6 kuanzia mwaka 2010 hadi 2015, kesi mpya 1,691 zilizofikishwa mahakamani zikiwemo kesi 227 zilizofikishwa mwaka 2010, kesi 193 (2011), kesi 288 (2012), kesi 343 (2013), kesi 256 (2014) huku kesi 384 zikifikishwa mahakamani mwaka 2015.
Aliongeza kuwa kesi zilizokuwa zinaendelea mahakamani kuanzia mwaka 2010 hadi 2015 zilikuwa 3,321 huku washitakiwa walioachiwa huru na mahakama katika kipindi hicho wakiwa 646.
Kwa upande wa kesi za rushwa zilizoondolewa mahakamani kutokana na sababu mbalimbali kuanzia mwaka 2010 hadi 2015 zilikuwa 162 kati ya hizo mwaka 2010 zilikuwa kesi 30, mwaka 2011 kesi 26 na mwaka 2012 kesi 24.
Kwa mwaka 2013 kulikuwa na kesi 17 zilizoondolewa mahakamani,wakati mwaka 2014 zilikuwa kesi 33 huku mwaka 2015 zikiwa kesi 32.
Mbali na kesi hizo, Kamishna Mlowola alisema kuanzia mwaka 2010 hadi 2015 kesi 54 zilikatiwa.
Kamishna Mlowola alimtaka kila mwananchi kutekeleza jukumu lake la kikatiba na kisheria katika kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa nchini.
Kifungu cha 39 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007 kinatamka kuwa “kila mtu anayefahamu kutendeka kwa kosa au anafahamu kusudio la mtu mwingine kutenda kosa chini ya Sheria hii anatakiwa kutoa taarifa TAKUKURU”.
“Hivyo, tunamsihi kila Mtanzania asijiingize katika vitendo vya rushwa na asinyamaze anapofahamu kutendeka kwa vitendo hivyo au hata kuwa na wasiwasi na mali zinazomilikiwa na mtu yeyote.” Alisema.
Alifafanua kuwa njia mojawapo nyepesi ya kuifikia TAKUKURU ni kupiga simu bure kwenda namba 113 au *113# (USSD) na kutoa taarifa za rushwa kwa muda wote wa saa 24.
Akizungumzia jinsi ya kukabiliana na vitendo vya rushwa, Kamishna Mlowola alisema ni wajibu kwa kila mwananchi kuzuia rushwa kwa kujijengea uelewa wa taratibu za eneo analokwenda kupata huduma na kupambana na rushwa kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa vinavyotokea au vilivyotokea ili hatua za kisheria zichukuliwe.
Post a Comment