Majambazi wapatao 10 juzi usiku walivamia magari mawili yaliyobeba wafanyabiashara waliokuwa wakitokea mnadani na kumuua kwa risasi, dereva aliyegoma kuwapa fedha na simu.
Dereva huyo, Chrispin Inyangwe (40) alipigwa risasi ya mgongoni alipojaribu kupambana nao.
Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana eneo la katikati ya vijiji vya Miula na Kalundi vilivyopo Kata ya Kipande wilayani Nkasi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, George Kyando alisema wafanyabiashara hao walikuwa wakitokea mnadani na walipofika eneo hilo walikuta mawe yamepangwa barabarani kuzuia magari.
Alisema baada ya kuona mawe hayo, magari hayo yalilazimika kusimama na ndipo majambazi hao waliokuwa na silaha za moto, mapanga na marungu walipoibuka na kufyatua risasi hewani na baadaye kutaka wafanyabiashara hao wasalimishe fedha na simu zao za mkononi.
Kamanda huyo alisema baadhi ya wafanyabiashara walisalimisha fedha na simu zao, na waliokataa walishambuliwa.
Inasemekana kwamba Inyangwe ambaye alikuwa dereva wa gari aina ya Mitsubishi Canter alikaidi kutoa fedha na kutaka kupambana nao, ndipo watu hao waliokuwa na bunduki aina ya SMG walipomfyatulia risasi iliyompata mgongoni na kufariki dunia papo hapo.
Kitendo hicho kiliwafanya wafanyabiashara wengine waliokuwa wakikataa kutoa fedha, kuzisalimisha sambamba na simu zao, ndipo majambazi hao walipowaachia na kukimbia.
Watu 19 waliojeruhiwa walipelekwa Hospitali ya Mkoa mjini Sumbawanga. Kamanda Kyando alisema majeruhi 12 waliruhusiwa kurejea nyumbani na wengine saba wanaendelea na matibabu na kwamba polisi wanaeendelea na msako wa watu hao.
Post a Comment