KAMPUNI ya Udalali ya Fosters Auctionare imesema bado Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) halijawapa taarifa zaidi kuhusu kuuza mali zilizokuwa katika ofisi za Kampuni ya Freemedia katika jengo lililokuwa limepangishwa na Freeman Mbowe akidaiwa Sh bilioni 1.172.
Ofisi hizo zilitumika kwa uchapishaji wa gazeti la Tanzania Daima na ukumbi wa disko wa Billicanas ambao Septemba mosi, madalali hao wakiwa na watumishi wa Kitengo cha Madeni cha NHC walitoa samani mbalimbali pamoja na vifaa vilivyokuwamo na kuvitoa nje.
Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Joshua Mwaituka alisema leo ndio siku 14 zinaisha tangu walipochukua mali hizo, lakini hawajapata idhini kutoka NHC juu ya kuuza mali hizo.
“Kwa utaratibu kampuni inapomaliza kukusanya mali za mdaiwa, huzihifadhi katika ghala letu lililopo Buguruni na ndani ya siku 14 huviuza, ikiwa tutakuwa tumepata idhini kutoka kwa mamlaka husika,” alisema Mwaituka na kuongeza kuwa NHC bado wako kimya.
Hata hivyo, alisema amepata taarifa kutoka vyombo vya habari kuwa lipo zuio la Mahakama kuhusu uuzwaji wa mali hizo, lakini NHC haijawasiliana naye kumpa taarifa zaidi.
Kwa upande wa NHC, hawakupatikana katika simu ili kutoa taarifa zaidi kuhusu suala hilo. Septemba Mosi, Kampuni ya Foster Auctionare ilifika katika ofisi hizo zilizopo katika jengo lililopo mtaa wa Mkwepu na Indira Gandhi na kutoa samani mbalimbali pamoja na vifaa vilivyokuwamo na kuvitoa nje.
Hata hivyo, Septemba 8, 2016, Mahakama Kuu ilizuia kupigwa mnada kwa vifaa na mali hizo kwa madai ya kuwepo kwa mzozo wa kodi ya pango baina ya kampuni hiyo na NHC.
Loading...
Post a Comment