Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Profesa Sifuni Mchome amesema kuanzia sasa sheria zote zitakazotungwa nchini zitakuwa katika lugha ya Kiswahili ili kuwawezesha wananchi wengi ambao ndio walengwa wa sheria hizo, kuzielewa.
Uamuzi huo unakwenda sambamba na kuzitafsiri sheria zote zinazotumika nchini ambazo ziko katika lugha ya Kiingereza ili kutimiza lengo hilo la kuwafanya wananchi wengi wazielewe.
“Kwa sasa serikali imeamua kuwa sheria zote nchini zitakuwa katika lugha ya Kiswahili na zile ambazo ziko katika lugha ya Kiingereza zitatafsiriwa ili kuwawezesha Watanzania wengi ambao ndio walengwa wa sheria hizo kuzielewa,” alisema.
Pia alisema serikali itazifanyia marekebisho sheria zote ambazo zimekuwa zikilalamikiwa na wadau mbalimbali kuwa hazikidhi mahitaji au haja, haziendani na wakati uliopo sasa ili kutekeleza azma yake ya kuwahudumia wananchi wake kwa ukamilifu.
Profesa Mchome ameyasema hayo jijini Dar es Salaam jana baada ya kupokea mapendekezo yaliyowasilishwa na Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (WILDAF), ambayo yanataka kufutwa kwa sheria mbalimbali za kimila zinazosimamia masuala ya mirathi ambazo zinalalamikiwa kuwakandamiza wanawake nchini.
Profesa Mchome amewashukuru WILDAF kwa kazi waliyoifanya na kuwaahidi kuwa wataalamu wake wizarani watayafanyia kazi mapendekezo yao ili kuhakikisha gurudumu la sheria nchini linasonga mbele na kuwasaidia wananchi wengi.
Akizungumza katika makabidhiano hayo Mkurugenzi wa WILDAF, Judith Odunga alisema mapendekezo hayo yanataka kufutwa kwa sheria za kimila ambazo kwa kiasi kikubwa zimekuwa zikiwakandamiza wanawake, kuwanyima haki ya kumiliki mali na kufanyiwa vitendo vya kidhalilishaji pale wanapofiwa na waume zao.
Alisema katika mapendekezo hayo WILDAF inaiomba serikali itunge sheria moja ambayo pamoja na zile za kidini itashughulikia masuala ya mirathi na kuweka usawa wa kisheria katika urithi wa mali kati ya mwanamke na mwanamume, ikiwa ni pamoja na watoto wa kiume na wa kike kuwa na usawa katika kurithi mali inapotokea mzazi wa kiume amefariki dunia.
Post a Comment