TAASISI ya Trade Mark East Afrika (TMEA) imetoa msaada wa dola za Marekani milioni 61 (Sh bilioni 132) kwa Mamlaka ya Bandari (TPA) kwa ajili ya kuboresha miundombinu mbalimbali ya Bandari ya Dar es Salaam pamoja na kuimarisha maeneo ya kuhifadhia makasha.
Hafla ya kusaini makubaliano ya msaada huo ilifanyika jana, Dar es Salaam kati ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Deusdedit Kakoko na Mkurugenzi Mkazi wa TMEA, John Ulanga.
Mradi huo utatekelezwa kuanzia Januari mwakani na kukamilishwa mwaka 2019.
Awali akizungumza, Ulanga alisema msaada huo utaboresha na kupanua kina cha bahari ili kuwezesha meli zenye uzito mkubwa kuweza kutia nanga katika bandari hiyo.
Aidha itawezesha kuwapo kwa marekebisho mbalimbali ya miundombinu ili kuongeza ufanisi katika shughuli za upitishaji mizigo bandarini, tofauti na ilivyo sasa.
Kwa upande wake, Kakoko alisema asilimia 90 hadi 95 ya mizigo hupitishwa bandarini hapo kwa mwaka na kwamba msaada huo utawezesha kuingiza meli zenye ukubwa na upana wa mita 261 tofauti na sasa ambapo ni meli zenye ukubwa wa mita 255 pekee zinazotia nanga.
Kakoko alisema TPA kwa sasa inapokea meli zenye uzito wa tani milioni 15 na baada ya maboresho hayo, itakuwa na uwezo wa kupokea mizigo yenye uzito wa tani milioni 26.
Loading...
Post a Comment