SERIKALI imesema kuwa maji upatikanaji wa maji katika mkoa wa Dar es Salaam umefikia asilimia 72 na kwamba Mpango wa Maendeleo ya sekta hiyo wa miaka mitano ijayo utawezesha kufikia asilimia 95.
Kwa upande wa vijijini, maji yanapatikana kwa asilimia 72 sawa na Dar es Salaam, huku mijini yakipatikana kwa asilimia 86 na katika wilaya yanapatikana kwa asilimia 60.
Hayo yalibainishwa juzi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Mbogo Futakamba, wakati akihojiwa kwenye kipindi cha Tunatekeleza kinachorushwa na TBC 1.
Futakamba alisema katika awamu ya kwanza ya mpango huo, walifanikiwa kutekeleza miradi 1,310 na kwamba Julai mwaka huu wameanza mradi huo wa pili wa kuhakikisha upatikanaji wa maji vijijini, mijini, usafi wa mazingira na utunzaji wa rasilimali za maji.
“Tunahakikisha kwamba kila Mtanzania anapata majisafi na salama na hii sekta ichangie katika ukuaji wa uchumi kupitia sekta ya viwanda. Hizi takwimu ni sahihi kwani tumetumia zile za Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) zilizoonesha ni kwa namna gani watu walifikiwa na huduma hiyo,” alisema.
Alifafanua kuwa vitu vinavyokwamisha utekelezaji wa miradi hiyo ni changamoto mbalimbali, ikiwemo uwekezaji katika miundombinu hiyo, uharibifu na mfumo wa chini wa upatikanaji wa maji kuwa ya chumvi hivyo hakuna wananchi ambao wako tayari kutumia.
Alisema kwa Dar es Salaam, maji yanapatikana lita zaidi ya milioni moja kutoka Ruvu Juu huku Ruvu Chini ikitoa maji zaidi ya lita milioni 270.
Akizungumzia mradi wa Kidunda uliopo Morogoro ambao pia utasambaza maji kwenye mikoa ya Pwani, Morogoro na Dar es Salaam, alisema utekelezaji wake umefanyika na unasaidia kudhibiti mafuriko, kupeleka maji katika mto Ruvu.
Alisema masuala ya kitaalamu yamekamilika. Aliongeza kuwa pamoja na kuweka sheria kwa watu wanaoharibu miundombinu hiyo, wameanzisha jumuiya za watumiaji maji ambao wanapewa mafunzo ya kuangalia masuala ya utawala, utunzaji fedha na utunzaji miundombinu na kudhibiti uharibifu ambao mara nyingi hufanywa na wananchi.
Kwa mujibu wa Futakamba, hali hiyo imesaidia sana kwa kuwa wananchi wanajua kwamba huo ni mradi wao na ukitokea uharibifu wanakuwa tayari kufanya matengenezo katika maeneo yaliyoharibiwa.
Loading...
Post a Comment