Loading...
Vita dhidi ya Dawa za Kulevya ..... UVCCM yatoa neno zito
Na Mwandishi Wetu. Kilimanjaro.
Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umesema haufurahishwi kuliona kundi la vijana aidha likijihusisha na uuzaji au utumiaji wa dawa za kulevya zinazopelekea Taifa kupoteza nguvu kazi na kudhoofisha dhamira ya kuyafikia malengo ya kiuchumi na maendeleo.
Pia Umoja huo umevitaka vyombo vya dola kuhakikisha wanafanya kila linalowezekana kukomesha uingizaji wa dawa za kulevya nchini na kuwakatama wauzaji papa wa biashara hiyo.
Kaimu Katibu Mkuu Shaka Hamdu Shaka ameyasema hayo jana mara baada ya mazishi ya Mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Hai Anold J. Swai alipotakiwa na waandishi wa habari kutoa kauli ya UVCCM kuhusiana na Sakata la dawa za kulevya lililoibuka hivi karibuni nchini, na kueleza jinsi UVCCM inahuzunishwa na tabia ya vijana kujiingiza katika kutumia dawa za kulevya.
Shaka alisema ikiwa vyombo dhamana vilivyokabidhiwa kupambana na dawa za kulevya wakiwemo polisi, kikosi cha kupambana na mihadarati au mahakama vikishindwa kuonyesha nia thabit, tatizo hilo kiuhalisia halitamalizika.
"Hatukuanza kusema leo, jana au juzi, mara kadhaa tumekuwa tukivitaka vyombo vya dola kuwakamata mateja wanaobembea kwenye vituo vya daladala na mitaani, waseme wamepata wapi dawa, ukimkamata mmoja, atamtaja mwingine na wengine zaidi watakamatwa "Alisema Shaka.
Aidha alieleza kuwa ikiwa vyombo dhamana ya kukamata na kudhibiti au vile vinavyotoa hukumu za kisheria vikichezewa kwa fedha za wauza unga, janga hili halitakwisha na vyombo hivyo kimsingi havitakuwa na hadhi stahili katika jamii.
"Kwanini polisi washindwe kuwakamata wauza unga, kama muuzaji amekamatwa na mzigo ukathibitika kweli ni unga, anawezaje kupata dhamana au mahakama imuachie mtu huyo kuwa huru na ofisi ya muendesha mashtaka ifute shitaka hilo "Alihoji Shaka.
Kaimu Katibu Mkuu alisema hadithi ya kwamba uuzaji wa biashara ya unga kwamba haiwezi kumalizwa kwasababu ati baadhi ya wahusika wake ni vigogo au watu wazito , hayana maana yoyote badala yake kila mmoja sasa aonyeshe kuchukizwa na biashara hiyo.
"Ikiwa baadhi ya polisi nchini, vikosi vya kupambana na dawa za kulevya, waendesha mashitaka, mahakimu na majaji hawatakubali kupokea rushwa na kusimamia sheria, janga hili litamalizika kufumba macho na kufumbua "Alisema Kiongozi huyo wa vijana.
Akitoa mfano Shaka alisema katika halmashauri za wilaya kuna ocd na polisi wake wakiwemo wapelelezi , mkuu wa wilaya ana maafisa wake, yupo Afisa mtendaji kata na mgambo, haiwezekani hawa wote wasijue wapi kuna mihadarati na nani anayeingiza na kuuuza ?" Alisema Shaka .
"UVCCM tunaunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk John Pombe Magufuli kutekeleza ilani ya uchaguzi kwa vitendo hasa katika maeneo nyeti yanayogusa uhai na mustakabali wa vijana katika taifa, ni wazi kuwa tukikaa kimya au kufumbia macho ukatili huu, kizazi hiki na kijacho kitaangamia, vijana sasa wanateseka unapowakuta wakitumia unga, nani anayewauzia, yupi anayeagiza na aliupitsha wapi hadi ufike mijini na vijijini Mhe Rais Magufuli ameonesha utayari wake katika vita hii kwa vile hakuna anaefurahia kuona taifa likiangamia"Alieleza
Shaka alisema ikiwa unga unafika na kusambazwa hadi maeneo ya vijijini, hakuna kijana atakayesoma, atakayelima, kuvua, kufuga au kufanya shughuli za uzalishaji mali hivyo Taifa litajikuta halina wataalam wa kuwategemea.
Hata hivyo Shaka amewaomba wananchi wote kutoa ushirikiano mzuri kwa vyombo vya ulinzi na usalama ili kutokomeza matumizi ya dawa za kulevya kwa kuwafichua watumiaji, wauzaji na waagizaji.
End
Post a Comment