Aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT), Sophia Simba CCM), amevunja ukimya na kusema hana mpango wa kuhamia chama chochote pinzani huku akisema adhabu aliyoipewa na chama hicho ameipokea kwa mikono miwili na hana kinyongo na chama hicho.
Sophia alitoa kauli hiyo Jumatatu katika mahojiano maalumu na Gazeti la MTANZANIA yaliyofanyika nyumbani kwake jijini Dar es Salaam.
“Kwanza una bahati msimamo wangu ni kutozungumza na waandishi wa habari ila kwa kuwa ni wewe haya. Kuhusu adhabu ya chama binafsi nimeipokea kwa mikono miwili na sina kinyongo na uamuzi wa chama changu hata kidogo. Ninajua wapo waliozusha, eti baada ya uamuzi wa Dodoma nimekwenda kukutana na mwanasiasa mmoja wa upinzani, taarifa hizi si za kweli na sitofanya hivyo, nimetoka Dodoma na kurejea hapa nyumbani kwangu Dar es Salaam nimepokewa na watoto wangu, ndugu na marafiki zangu.
Aliongeza “Napenda kuwaeleza Watanzania wote, wafahamu sina mpango wa kujiunga na chama chochote cha upinzani. Na unajua CCM ina makundi mawili, la kwanza ni wanachama wenye kadi na la pili wakereketwa ambao ni wengi nami nitaingia katika kundi hilo na si kuhama,” alisema Sophia.
Post a Comment