Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

Sukari yaibua mjadala mzito Bungeni

SAKATA la sukari limeibuka tena bungeni baada ya Jaku Hashim Ayoub, mbunge anayewakilisha Baraza la Wawakilishi (CCM), kuitaka serikali kueleza utaratibu unaotumika kutoa vibali vya kuingiza bidhaa hiyo nchini.

Mbunge huyo aliliibua suala hilo wakati wa kipindi cha 'Maswali kwa Waziri Mkuu' bungeni mjini hapa jana, huku akitilia shaka upatikanaji wa bidhaa hiyo wakati wa mfungo wa mwezi wa Ramadhan.

"Unakaribia mwezi Mtukufu wa Ramadhan, kama wiki mbili panapo majaliwa tukifika, na hali ya kusikitisha mwezi Mtukufu wa Ramadhan sukari inahitajika sana," alisema.

"Hata wananchi wa Ruangwa, Peramiho, wanahitaji sukari, na Mwenyezi Mungu alitupa mtihani wa mvua, viwanda vyetu vya ndani havikuzalisha sukari ya kutosha na uchunguzi wa harufu niliyoipata tunahitaji kama tani 100,000... lakini cha kusikitisha taarifa niliyokuwa nayo wametoa vibali vya tani 300,000.

"Sasa hawa mliowapa vibali, sukari yao hata ikifika Ramadhan ishakwisha itawasaidia nini wananchi? Je, mnatumia utaratibu gani kuwapa vibali hawa watu? Je, ni wale wale, au wengine?" Alihoji.

Katika majibu yake, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alisema serikali inalifuatilia kwa kina suala hilo na imeandaa mkakati wa kuongeza uzalishaji wa bidhaa hiyo ili kutatua changamoto iliyopo.

"Napenda niwathibitishie Watanzania kwamba, serikali iko macho na inajua ni maeneo gani ambayo yanahitaji kuboreshwa kulingana na mahitaji ambayo yanahitajika," alisema.

Waziri Mkuu alikiri Tanzania haina uzalishaji wa kutosha sukari wa kutosheleza mahitaji ya wananchi wake kwa kuwa katika mwaka wa kilimo mahitaji ya sukari nchini ni zaidi ya tani 420,000, lakini uzalishaji uliopo ni wa tani 320,000.

"Tuna upungufu wa sukari inayohitajika ya tani 100,000 na ukiwezekana ni zaidi kwa ajili ya ongezeko la watumiaji," alisema.

Alisema zaidi kuwa kila mwaka serikali ina utaratibu wa kuagiza sukari na safari hii imeagiza tani 131,000, wakizingatia takwimu zilizofanyiwa utafiti na Bodi ya Sukari (SBT).

Alisema kuwa, tayari wameshaagiza tani 80,000 na kati yake, tani 35,000 zimeshaingia na wameshaanza kuzigawa katika maeneo yote ya nchi ili kupunguza bei.

Katika kukabiliana na changamoto ya upungufu wa bidhaa hiyo wakati wa mfungo wa mwezi wa


Ramadhani, Waziri Mkuu alisema utaratibu wa kuagiza sukari zaidi kufikia malengo umeshaandaliwa.

Aliwaomba wananchi kushirikiana kuwasihi wafanyabiashara ambao hivi sasa wamepandisha bei bila sababu na kuwaumiza Watanzania, kupunguza bei hizo.

Alisema ipo mikakati ya kuongeza uzalishaji kufikia malengo kwa kuwa serikali inatambua uzalishaji wa viwanda vinne vya sukari wa Kagera, Kilombero, TPC na Mtibwa na cha tano kilichopo Tanzania visiwani.

"Tumejiwekea utaratibu wa kukutana na wafanyabiashara wa viwanda na kuwasihi kuongeza uzalishaji na tumeona jitihada kadhaa ambazo zinafanywa na wazalishaji wa sukari," alisema Majaliwa.

"Kwa bahati nzuri sana wiki moja iliyopita nilikuwa mkoani Kilimanjaro na kupata nafasi ya kutembelea kiwanda cha TPC ambacho kimeonesha mafanikio makubwa ya uzalishaji zaidi, ambapo mwaka jana walizalisha tani 100,000 na sasa wameongeza tani 20,000," alisema.

"Pia nilipofanya ziara mkoani Manyara, nilitembelea Manyara Sugar, kweli viwanda vingi vinaendelea kujengwa na sasa tunakamilisha taratibu za kuanza ujenzi wa kiwanda cha sukari mkoani Morogoro, kuna eneo la Mbigili kwa ushirikiano wa Magereza.

"Lakini pia eneo la Mkulazi ambalo linaandaliwa na NSSF na PPF kwa pamoja na wawekezaji ambao wako tayari kuwaunga mkono katika uzalishaji wa sukari, hivyo nataka niwatoe mashaka Watanzania sukari ipo na wakati wa Ramadhan sukari ya kutosha itakuwapo, wala hakuna sababu ya kuongeza bei.

Tutafanya ufuatiliaji kuona bei haziongezeki."

Upungufu wa sukari nchini ulitikisa Bunge mwaka jana, huku baadhi ya wabunge wakipinga uamuzi wa serikali wa kusitisha vibali vya uingizwaji wa bidhaa hiyo nchini.

Aidha, Katibu Mtendaji wa Chama cha Wazalishaji Sukari Tanzania (TSPA), Deo Lyatto aliiambia Nipashe kwa njia ya barua pepe mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa viwanda vya sukari nchini vilizalisha tani 326,909 mwaka jana kulinganisha na tani 293,146 za msimu wa 2015/16, imeelezwa.

Msimu wa uzalishaji sukari huanza Mei na kufungwa Aprili ya mwaka unaofuatia.

Uzalishaji huo, alisema Lyatto, ni sawa na ongezeko la tani 33,763.
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top