Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Kunti Majala amesafirishwa chini ya ulinzi wa polisi leo kutoka Chemba hadi ofisi za polisi mkoa wa Dodoma kwa ajili ya kuhojiwa akidaiwa kuanza kampeni za uchaguzi mkuu ujao mapema.
Kwa mara ya kwanza, Kunti alikamatwa katika Kijiji cha Mapango Kata ya Chandama wilayani Chemba juzi akidaiwa kufanya kusanyiko lisilo halali.
Akizungumza jioni ya Jumatano, Julai 19, Kunti amesema alienda kuripoti Kituo cha Polisi Chemba leo saa 2.00 asubuhi kama alivyotakiwa juzi na polisi baada ya kuhojiwa kwa zaidi ya saa tatu.
Hata hivyo, amesema baada ya kuripoti kituoni hapo alichukuliwa na gari la polisi hadi ofisi za mkoa za jeshi hilo kwa ajili ya mahojiano zaidi.
"Tangu saa 2 asubuhi ndio sasa wananiachia saa hizi (saa 1.30 jioni) niende nyumbani baada ya mahojiano. Wameniambia wakinihitaji wataniambia," amesema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa amethibitisha kusafirishwa kwa mbunge huyo hadi Dodoma kwa ajili ya mahojiano.
Amesema imebainika kuwa mbunge huyo ambaye aligombea ubunge katika jimbo hilo mwaka 2015, ameanza kufanya kampeni za kuomba kuchaguliwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 kupitia mikutano yake ya kisiasa.
Juzi, mbunge huyo alihojiwa na polisi na kutakiwa kuripoti tena leo kwa madai ya kutoa lugha chafu dhidi ya Serikali.
Post a Comment