Dk. John Pombe Magufuli, Rais Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Vifaa vya tiba vya kisasa kabisa katika moja ya Hospitali hapa nchini
*****
Mara baada ya kupata Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961 Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alitangaza vita dhidi ya maadui watatu ambao ni ujinga, maradhi na umaskini. Mwalimu Nyerere alisema wazi kuwa ili Taifa letu liendelee halina budi kupambana dhidi ya maadui hao.
Kwenye mapambano dhidi ya 'ujinga' tumeshuhudia Serikali ikijenga shule za msingi kwenye kila kijiji na mtaa, Serikali ikijenga shule za sekondari kwenye kila kata; Serikali ikitoa elimu bure kuanzia ngazi ya shule ya msingi mpaka Sekondari; Serikali ikitoa mikopo ya elimu ya juu kwa wenye sifa vyuoni; Serikali ikiboresha miundo mbinu ya maabara, maktaba na madawati; Serikali ikihakikisha Waalimu wanakuwepo wa kutosha na wakiwahudumia kwa kuwapatia mishahara na makazi.
Upande wa mapambano dhidi ya umaskini Serikali imekuwa ikitoa ajira rasmi na zisizo rasmi; Serikali inaboresha kilimo kuwa cha kibiashara na chenye tija zaidi; kujenga viwanda; kuhimiza uwekezaji nchini; kuboresha mikataba ya madini n.k
Hata kwenye upande wa adui maradhi mapambano ya adui huyu bado ni makali Serikali ikijitahidi kumshinda.
Katika vipindi mbalimbali tumeshuhudia Serikali ikijenga vituo vya afya, zahanati na hospital kwenye maeneo mbalimbali nchini; kujenga hospitali ya Moyo nchini ambapo inafanya mpaka upasuaji mkubwa wa moyo.
Tumeshuhudia Serikali ikiendelea kununua vifaa tiba, mashine, vitanda, kupambana na maleria, kifua kikuu, ukimwi na magonjwa mengineyo hatarishi.
Serikali imeboresha kwa kiwango kikubwa huduma ya uzazi ya Mama na Mtoto na kujivunia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.
Pamoja na mambo mazuri Serikali inayoendelea kufanya kuboresha sekta ya afya nchini kulikuwa na matatizo makuu mawili upande wa madawa. Mosi; Tatizo sugu la upatikanaji wa madawa nchini ambapo kwenye hospitali za Serikali hazipatikani licha ya kuwa zilikuwa zinapelekwa na mgonjwa akiandikiwa dawa anaambiwa akanunua duka la nje la hospitali ya Watu binafsi.
Tumeona jitihada za dhahiri za Serikali za kujenga maduka ya madawa ndani ya hospitali ambapo jukumu hilo la ujenzi na usimamizi wamepewa MSD na sasa dawa zinapatikana ndani ya hospitali na sio tena kuagizwa kwenda kununua maduka ya nje.
Pili; Kulikuwa na tatizo la dawa kuuzwa kwa bei kubwa na hivyo kumfanya mtu wa hali ya chini kushindwa kumudu gharama za ununuzi wa madawa.
Hivi karibuni Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu jijini Dar es salaam alipokuwa akizungumza na wafanyakazi wa Bahari ya Dawa (MSD) amesema Serikali imesema kuwa imepunguza bei ya vifaa mbalimbali vinavyotumika katika sekta ya afya zikiwemo bei za dawa, vitendea kazi na vifaa tiba vya maabara vinavyonunuliwa na kusambazwa na Bohari ya Dawa(MSD) kwa asilimia 15. Mfano sasa Serikali wamepunguza kodi kwenye dawa mpaka asilimia 67 (67%) hali iliyopelekea kupunguza zaidi bei za dawa nchini.
Hayo ni matokeo ya utaratibu wa ununuzi wa moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji kama Rais Dkt. John Magufuli alivyowagiza Wizara ya Afya kufanya na sio kununua tena kwa mawakala.
Hakika, hii ni habari njema kwa Watanzania waliokuwa wakiteseka kwa kutumia gharama Kubwa kununua madawa na ni habari mbaya kwa wale waliozoea ulanguzi wa bei za dawa. Hakuna tena sababu ya kulanguliwa wala mtu kufa kwa kukosa dawa.
Sio tu kodi za kwenye madawa zimepunguzwa bali hata kodi za kubebea Wagonjwa imetolewa kabisa.
Heko ziendee kwa Serikali ya Rais Magufuli kwa kuendelea kusimama na kuwa watetezi wa wanyonge nchini.
Na Emmanuel J. Shilatu
0767488622
Burhan awekewa vikwazo na Marekani
7 hours ago
Post a Comment