Mwanaume mmoja anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa kosa la kumteka mtoto wakike aitwaye Khailati Bashiri (8) ambaye ni mwanafunzi wa darasa pili katika Shule ya msingi ya Iloganzala mkoani Mwanza.
Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, DCP Ahmed Msangi amemtaja mtuhumiwa huyo kuwa ni Emmanuel Kirumbas (25) mkazi wa Malampaka mkoani Shinyanga ambapo majira ya 6:00 mchana ya tarehe 21.08.2017 alimchukua mwanafunzi huyo na kumpeleka kusikojulikana na baadae kutuma taarifa kwa njia ya simu kwamba apatiwe fedha kiasi cha Milioni 3 ili aweze kumrudisha mtoto huyo.
Inasemekana kuwa baada ya mtoto huyo kutoka shuleni alikwenda nyumbani kwao mtaa wa Iloganzala anapoishi na wazazi wake kubadilisha nguo kisha aliondoka na kuelekea kusikojulikana, na kusababisha wazazi wake kuhangaika kumtafuta bila ya mafanikio ndipo walipoamua kutoa taarifa kituo cha Polisi.
DCP Msangi amesema baada ya kupokea taarifa hizo jeshi la polisi lilifanya upelelezi ambao ulipelekea kuwakamata watu watano na baadae kufanikiwa kumkamata mtekaji nyara ambae alikuwa akihitaji kulipwa fedha.
Jeshi la Polisi lipo katika mahojiano na mtuhumiwa na pindi uchunguzi utakapokamilika mtuhumiwa aliyehusika na utekaji atafikishwa Mahakamani.
Post a Comment