Kama kuna jambo baya ambalo baadhi ya Watu
wanaoneka kulipenda sana nakuamini ni kuongopewa kwa maneno matamu ya kisiasa
ambayo huwa hayana uhai wala afya ya kuendelea huku Watu wengine wakishindwa
kumuamini au kumpenda mtu msemakweli asiyependa kuchezea akili zao kwa
kuwaongopea.
Maneno mengi ya kufurahisha hadharani aghalabu
huwa hayana mwisho mwema na wala huwa hayaleti tija au manufaa kwa jamii.
Waswahili husema ni heri mtu asemaye kweli na kutetea haki za wengi kuliko
anayeongopa kwa kutumia lugha tamu isioleta mafanikio.
Miongoni mwa viongozi wasema kweli ambao
hawapendi kudanganya Wananchi ni Rais John Pombe Magufuli. Kweli atasema
na kusimamia ukweli, njano atasema hii ni njano na wala siyo nyeusi. Kwa jambo
lisilowezekana kwa wakati husika hatamung'unya maneno ila yuko tayari
msimuelewe kwa wakati huo kuliko kuongopa.
Wote tunajua Rais wetu amejitolea muhanga
kupigania maslahi mapana ya Taifa letu huku akitaka rasilimali na maliasili za
nchi ziwanufaishe wananchi wote hususan watu masikini na wanyonge walioko
vijijini ambao wanaokosa huduma bora za jamii.
Ukiisikiliza kwa umakini hotuba ya Rais wakati
akizumgumzia kwenye mkutano wa 33 Jumuiya ya Serikali za Mitaa
Nchini (ALAT), utajua anajua jinsi michezo michafu ya fedha za umma
ambazo ni ruzuku toka Serikali kuu zilivyopotea au kutafunwa kiholela na
wajanja wachache kwenye halmashauri za wilaya.
Kwenye hotuba yake amehimiza na kuweka
msisitizo huku akiwataka watendaji wa halmashauri za wilaya, Wakurugenzi, Wakuu
wa idara na Madiwani, kuongozwa na shime ya uzalendo ili kuijenga nchi yetu kwa
kufuata sheria na kuheshimu misingi ya uaminifu, uadilifu, uwazi na
uwajibikaji.
Rais anaonekana dhahiri kutambua shida na
dhiki zinazowakabili Wafanyakazi, si wale tu walioko kwenye utumishi wa
umma peke yake. Anajua kuna Waganga na Wauguzi, Walimu wa shule za Msingi na
Sekondari, wataalam wa ugani kwa maana ya Mabwana na Mabibi shamba, Mabwana na
Mabibi afya, Wahandisi na Maafisa wa maendeleo ya jamii.
Kuna watumishi wa umma kwenye ngazi za Serikali
kuu na kwenye Serikali za Mitaa, Wafanyakazi wa Majumbani, Walinzi,
Madereva, Wahudumu wa baa na wanaofanya kazi kwenye hoteli za kitalii ambao pia
wanaolipwa ujira na mishahara hafifu.
Makundi yote hayo na mengine, kimsingi yanahitaji
kutazamwa kwa macho ya kusaidiwa na kulindwa haki zao chini ya usimamizi
wa Serikali kwa mujibu wa sheria ili waweze kupata stahili zao zitakazoweza
kuendesha maisha yao aidha wanapokuwa kazini au baada ya kustaafu.
Ili hayo na mengine mengi yaweze kufikiwa,
Serikali inahitaji kukusanya mapato kwa uhakika. Anataka kusiwe na upotevu
unaovujisha mapato hayo na kupotea hovyo lakini pia kile kidogo
kinachopatikana kilindwe ili kiwanufaishe Wananchi wote.
Nchi yetu kwa miaka mingi imepata pigo na matatizo
ya kuwepo kundi la mafisadi, wabadhirifu wa mali za umma, wezi na
matapeli waliokuwa wakipata vipato na kutajirika huku wakiiba fedha za Serikali
na kujinufaisha wao binafsi .
Leo kama Rais atasimama hadharani akatoa
maneno laini ya kisiasa ili kuwafurahisha watumishi kwenye Serikali za
Mitaa wakati yapo makundi mengine bado stahili zao hazijatizamwa na
kurekebishwa kimanufaa, huo utakuwa ni uongo mpya mweupe.
Katika maelezo yake amesema, anazungumza na
watumishi wa Serikali za mitaa si kwa lengo la kuwaongezea mishahara, huo ndiyo
ukweli. Aongeze mishahara kwa watumishi wa kundi hilo je watumishi wengine
watalipwa na nani?
Tuna Walimu wanaoishi vijijini wakiwa hawana
nyumba za kuishi, huko vijijni hakuna maji safi na salama, hawajui umeme
unawakaje, barabara ni mbovu hazipitiki, hawana zahanati, kama zipo
hazina Waganga na Wauguzi, zimekosa dawa na vifaa tiba huku kina mama
wajawazito wakipoteza maisha.
Mabwana na Mabibi shamba hawana nyenzo wala
usafiri, maafisa uvuvi na mifugo wakikabiliwa na upungufu mkubwa wa zana za
uendeshaji wa shughuli muhimu kwa Wananchi ili kuwapa taaluma aidha
katika sekta za uvuvi, kilimo cha kisasa na ufugaji wenye tija na manufaa.
Vijijini kina Mama Wajawazito na Watoto chini
ya umri wa miaka mitano wanahitaji chanjo na kinga, vifaa tiba na huduma
bora vya upimaji wa afya zao karibu kila wiki wakitakiwa kufika zahanati na
kliniki ili kujua maendeleo ya afya zao .
Vijijini wakulima hawapa pembejeo za kilimo na
mifugo kwa wakati muafaka, hawana zana za kisasa ikiwemo matrekta, hadi sasa
katika karne ya 21 watu bado wanatumia kijembe cha mkono kulima zaidi
ekari tano huku wajanja wachache wakitafuna fedha za umma na kujenga mahekalu
na nyumba za kifahari.
Katika Shule za Msingi na Sekondari huko
vijijini watu zinakabiliwa na upungufu wa madarasa, maabara, idadi ndogo
ya Walimu, hakuna mashimo ya vyoo, hawapati maji safi na
salama, kuna magonjwa ya milipuko kama kipindupindu, matumbo ya
kuharisha, malaria na maambukizi ya virusi vya ukimwi .
Rais anayejua shida, dhiki na matatizo ya Wananchi
wake katu hawezi kuwa muongo au mnafik wa kulifurahisha kundi moja la Wafanyakazi
ili wampigie makofi, nderemo na vigelegele vya uzandiki wakati kwenye maeneo
mengine ya nchi yake kuna shida kubwa na matatizo yasiyokadirika.
Rais Dk Magufuli amehimiza na kuwataka Watumishi
waliopewa dhamama za utendaji wakiwemo Madiwani, Wakurugenzi wa halmashauri za
wilaya na wakuu wa idara, kujali uzalendo na utaifa. Kulinda na kutunza vyema
fedha za umma na kuitumia vizuri kwa kadri ya miradi yote ilivyopangiwa,
kuidhinishwa na vikao utekekezaji wake utoe matokeo chanya.
Mataifa ya wenzetu kama China, Taiwan,
Malaysia, Vietnam, India, Dubai, Oman au Hong Kong, kwanza yaliweka kando siasa
, wakatupa pembeni maneno maneno na uongo hatimaye yakaongozwa na ukweli
hadi kufika mahali walipo sasa kimaendeleo kwa kujali uzalendo na dhima ya
kupigania maendeleo ya kiuchumi .
Kwa kukataa uongo na kwa kutambua hayo yote
Rais Dk Magufuli amesema Serikali yake itashughulikia mishahara ya Walimu na Wafanyakazi
wote, katika bajeti ijayo ataongeza mishahara ya kawaida kwa Wafanyakazi (annual
increments) maana ilisimama kwa muda mrefu.
Kwa kawaida na ada ya mtu msemakweli na
asiyependa uongo, amesimama na kusema analoliamini kuwa hajapandisha mishahara
na hatapandisha mishahara kwa wakati huu. Alichaguliwa ili kusaidia wananchi
wanyonge walioko vijijini na mijini nao wapate huduma bora. Jukumu la Rais yeyote
bora mwenye uzalendo ni kuweka mkazo katika utoaji wa huduma kwa wananchi
wote.
Kimsingi, kimantiki na kiuhalisia maneno hayo
hutamkwa na Rais mwenye nia na dhamira njema yenye muhimu au ulazima na
dhati ya kuyatazama maisha ya Wananchi wengi masikini, wanaokosa huduma bora,
wenye dhiki, shida na matatizo ya kukosa elimu ili kufuta ujinga, wanaondamwa
na adui umasikini pamoja na kusakamwa na maradhi .
Wapo wanasiasa waliozoea kuwadanganya wananchi
wakati wa kampeni na wengine hata kufikia kusema na kuahidi wakichaguliwa
watajenga mabomba yatakayotoa maziwa na asali, kujenga barabara za lami,
watakaotibiwa hapa hapa nchi huku wanapoumwa huenda nje ya nchi kwa matibabu na
wengine wapo waliodai wana uwezo wa kuleta mabadiliko ya kiuchumi wa siku
mia moja.
Pia wapo Waandishi wadaku, wakuda na wajuba
wasio na mioyo ya uzalendo ambao nao wameanza kupotosha maana na msingi wa
matamshi ya Rais ili kueneza na kuendeleza utamaduni wa kupika uongo kwa
jamii huku wakimlisha maneno ambayo hayakuyatamka .
Jambo muhimu kwa Watanzania wote, tutambue
kuwa wakati umefika tukatae maneno matamu ya kisiasa yenye siha hafifu na uongo
mwingi, afya duni ya muda mfupi huku tukibadilika na tukimtambua mtu msemakweli
na mwenye dhati ya kujenga Taifa la watu wenye lengo la kujikwamua na madhia ya
umasikini hatimaye kujitegemea.



Post a Comment