Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimewakilishwa nchini Uingereza na Ndg. Ngemela Lubinga Katibu wa NEC Mwenye dhamana ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa.
Ndugu Lubinga ameongoza ujumbe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Mkutano Mkuu wa Chama rafiki cha Labour. Katika Mkutano huo Chama cha Labour kimeweka mikakati ya kurejesha Chama hicho katika kushika hatamu ya uongozi nchini Uingereza.
Akiwakilisha salamu za Comrade John Pombe Joseph Magufuli, Mwenyekiti wa CCM katika Mkutano huo Ndg. Lubinga amesisitiza, *…ni lazima vyama rafiki na hasa vyenye mrengo wa kijamaa kusimama pamoja katika kuhakikisha usawa na haki inapokuja katika uvunaji wa rasilimali madini hasa katika nchi za Afrika.*
Katika mazungumzo yake na Viongozi waandamizi wa labour Ndg. Lubinga amewahakikishia mahusiano ya kidugu ambayo yamejengwa kwa muda mrefu kati ya vyama hivi viwili, CCM itaendelea kuyaenzi.
Aidha Ndg. Ngemela Lubinga alijulisha viongozi hao kuwa CCM inaendelea kufanya Mageuzi Makubwa ambayo lengo lake ni kurejesha Chama chetu katika misingi yake, kuuimarisha kwa vitendo uhalisia kwamba CCM ni Chama Cha wanachama na kinachoshughulika na shida za watu. *Kama sehemu ya Mageuzi haya ndani ya Chama na katika Serikali, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeielekeza Serikali kutoa elimu bure kutoka darasa la kwanza mpaka kidato cha nne na kuongeza maradufu mikopo kwa wanafunzi wote wenye uhitaji wanaosoma katika Vyuo Vikuu nchini* alisema Ndg. Lubinga.
Akihitimisha salamu za CCM katika Mkutano huo Mkuu wa Chama Cha Labour, Ndg. Lubinga Amewaasa wanachama na viongozi wa Chama Cha labour kuweka maslahi ya umma mbele na kushughulika na changamoto zao ikiwemo mahusiano ya Nchi ya Uingereza na Jumuiya ya Ulaya.
Nao viongozi wa Chama Cha Labour wamepongeza jitihada za Serikali ya CCM awamu ya Tano Chini ya Ndg. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuwa madhubuti katika vita dhidi ya rushwa, ubadhirifu wa mali ya umma na kutetea haki ya watanzania katika rasilimali madini.
Ziara hii ya Ndg. Lubinga Nchini Uingereza ni muendelezo wa diplomasia ya Siasa na ujenzi wa mahusiano mema na vyama rafiki.
Imeandaliwa na Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Imetolewa na,
*IDARA YA ITIKADI NA UENEZI
CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM)*
Novemba 6, 2017
on Monday, November 6, 2017
Post a Comment