Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Dodoma inamshikilia Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Sadifa Juma Khamis kwa tuhuma za kugawa rushwa kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa uchaguzi.
UVCCM leo Jumapili Desemba 10,2017 inachagua viongozi wapya wa ngazi ya Taifa watakaoongoza jumuiya hiyo ya CCM kwa kipindi cha miaka mitano.
Sadifa ambaye pia ni mbunge wa Donge, Zanzibar amekamatwa nyumbani kwake karibu na mnada wa zamani mkoani Dodoma.
Kamanda wa Takukuru mkoani Dodoma, Emma Kihanga amethibitisha kukamatwa kwa mwenyekiti huyo na kwamba watatoa taarifa zaidi baadaye.
"Ni kweli tumemkamata tangu jana usiku tumekesha tunafanya uchunguzi, nitatoa taarifa baadaye kuhusu tukio hilo," amesema.
Mkutano mkuu wa uchaguzi wa UVCCM unaendelea mjini Dodoma na miongoni mwa waliohudhuria ni Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli.
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan akifunga mkutano mkuu wa uchaguzi wa Umoja wa Wanawake (UWT) jana Jumamosi Desemba 9,2017 alisema hawajapokea malalamiko mengi kutoka umoja huo na kuzitaka jumuiya nyingine za CCM kujifunza UWT.
Post a Comment