*Na Emmanuel J. Shilatu*
Mara baada ya Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM kupitisha majina ya Dk. John Magufuli kugombea nafasi ya Mwenyekiti CCM Taifa, Dk. Ali Mohammed Shein kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti CCM Tanzania Zanzibar, na Ndugu Philipo Mangula kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti CCM Tanzania Bara nikaandika makala kuwapongeza kwa uamuzi wao huo na kuwaomba Wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM Taifa kuwapa kura za kishindo ikiwezekana asilimia 100.
Hakika! Maombi yangu, ya wana CCM na ya Watanzania wengi waliokuwa wakitaka ushindi wa kishindo yametimia. Rais Dkt John Magufuli amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Rais Shein Makamu Mwenyekiti Zanzibar na Philip Mangula Makamu Mwenyekiti Bara na Kanali Abdulrahman Kinana kuwa Katibu Mkuu wa CCM Taifa.
Matokeo ya kura za Mwenyekiti wa CCM Taifa. KURA Zilizopigwa 1821, Halali 1821, Zilizoharibika 0, Hapana 0, Ndiyo 1821, Mwenyekiti CCM Taifa, Rais Dk. Magufuli.
Matokeo kura za Makamu Mwenyekiti CCM Bara. KURA Zilipopigwa- 1827, zilizoharibika- 1, halali- 1826, Ndiyo- 1826, Makamu Mwenyekiti CCM Bara, Phillip Mangula.
Matokeo ya kura za Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar. KURA Zilizopigwa 1821, Halali 1821, Zilizoharibika 0, Hapana 0, Ndiyo 1821, Makamu Mwenyekiti CCM Zanzibar, Rais Dk. Shein.
Ni ushindi wa kishindo! CCM inazidi kujionyesha kuwa ni Baba wa Demokrasia Afrika. Chama Cha Mapinduzi ndio chama pekee hapa nchini ambacho kinatoa uhuru wa nafasi ya Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti Taifa kuweza kuchaguliwa kwa ushindani wa kupigiwa kura tofauti na ambavyo udikteta ulivyotamalaki kwenye vyama vingine vya kisiasa ambavyo nafasi ya Mwenyekiti au Makamu Mwenyekiti haiojiki na huwa maalum kwa Watu maalum hata akikaa kwa muda mrefu si kitu kwao.
Wapo waliokuwa wakihoji Dk. Magufuli alikuwa akigombea na nani? Wanaohoji hivyo, wanasahau kuwa Tangu mwaka 1992 - 2003 Freeman Mbowe alikuwa ndiye mwenyekiti wa kurugenzi ya Vijana ya Chadema, Mpaka leo hii wameshindwa kutuambia Mbowe alikuwa akigombea na nani nafasi hiyo.
Pia wangetueleza mwaka 2004 na mwaka 2009 Mbowe alikuwa akigombea na nani nafasi ya Uenyekiti wa Chadema alioupata? Mambo mengine walipaswa wajitathmini kwanza ndipo wapate uhalali wa kuhoji.
Kama haitoshi mwaka 2015 Lowassa alishindanishwa na nani hadi akapewa fursa ya kugombea urais kupitia Chadema kwa mwamvuli wa Ukawa? Tulichokiona ulikuwa uhuni wa kusema ndiooooo na wala si demokrasia ya kushindanishwa na wengineo kwenye sanduku la kura.
Pasipo kusahau, Kwa mujibu wa katiba na kanuni za uchaguzi ndani ya Chadema. Katika mchakato wa kumtafuta katibu mkuu mpya, mwenyekiti alipaswa kuwasilisha mawili ya watu wanaopendekezwa na kamati kuu kwa nafasi ya ukatibu mkuu ili mkutano mkuu uwapigie kura na kumpata mmoja.
Lakini tar 12/3/2016 kule Mwanza, mwenyekiti alikuja na jina moja mfukoni na kazi yao ilikuwa kupiga kura ya ndiyo au hapana, pamoja na kupiga picha tu pale Gold Crest Mwanza. Sasa kawaulizeni Dr Mashinji alishindanishwa na nani katika kura kama haikuwa Ndiyo na Hapana?? Je bado kura ya ndiyo au hapana siyo demokrasia?
Narudia tena kuwapongeza Wajumbe mkutano mkuu wa CCM kwa uamuzi wa busara wa kumchagua kwa kishindo Dk. Magufuli kuwa Mwenyekiti wa CCM Taifa. Katika utawala wa Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Magufuli tumeshuhudia;-
1. Utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) 2015 – 2020 kwa kiwango kikubwa unaofanywa na Serikali iliyopo madarakani. Jambo lililo jema Chama kimekuwa mstari wa mbele kusimamia utekelezaji huo wa ilani ya uchaguzi.
2. Ndani ya kipindi kifupi kumefanyika mabadiliko ya kweli kwenye chama yaliyopunguza gharama, urasimu na vyeo kumilikiwa na wachache. Hivi sasa Chama kimekuwa kimbilio kubwa la Wanyonge wengi ambao hivi sasa wamepata fursa ya kushinda uchaguzi ndani ya CCM. Hakika Wanyonge walio wengi wapo began a Rais Magufuli.
3. Chama kikirudishwa kwenye misingi yake iliyoasisiwa toka TANU na ASP ambapo CCM asili yake ni chama cha Wakulima na Wafanyakazi, uchaguzi wa mwaka huu Wanyonge wengi wameshinda na kushika nafasi kubwa kubwa. Wanyonge wengi wenye uweledi na kisomo wamekuwa wakipata fursa za kiuteuzi ndani ya Serikali na chama pia.
4. CCM kikirudi na kufuata misingi ya Azimio la Arusha. CCM ya leo inapigania sana suala la haki, usawa, na kukemea vikali mambo ya rushwa na ufisadi ndani ya chama na Serikali yaliokuwa yakileta urasimu, matabaka na manyanyaso kwa jamii. Hali hiyo imekifanya Chama Cha Mapinduzi kuwa kipindilio na mahali salama kwa Wanyonge waliokuwa wakiteswa na Matajiri waliokuwa wakitumia pesa zao kuwanyanyasa.
Kwa haya, Dk. Magufuli ataendelea kuungwa mkono mno na asilimia kubwa ya Wanyonge. Tuendelee kushangilia ushindi wa Dk. Magufuli, tuendelee kujifunza demokrasia ya kweli ndani ya CCM.
*Na Emmanuel J. Shilatu*
Post a Comment