Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

MJUE RAIS WA ZIMBABWE MHE. MNANGWAGWA ANAYEWASILI LEO


Rais wa Zimbabwe Mheshimiwa Emmerson Dambudzo Mnangwagwa (pichani) atarajiwa kuwasili nchini leo tarehe 28/Juni/2018 mda wa saa 5 asubuhi hii kwa ziara ya kikazi na kulakiwa na Mwenyeji wake Rais John Pombe Magufuli.

Hii ni ziara ya kwanza kwa kiongozi huyo nchini Tanzania tangu aapishwe kuongoza nchi ya Zimbabwe kama Rais wa Tatu na mkuu wa dola,serikali na amiri jeshi mkuu mnamo tarehe 24/Novemba/2017 kufuatia kujiuzuru kwa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Robert Mugabe aliyeiongoza Zimbabwe kwa takriban miaka 37.


Rais mstaafu Robert Mugabe alijiuzuru nafasi hiyo kufuatia shinikizo la chama chake cha ZANU-PF kinachotawala nchi hiyo baada ya Bunge la Zimbabwe kudhamiria kumpigia kura ya kutokuwa na imani nae huku jeshi likizingira maeneo yote muhimu ikiwemo ikulu. 


Rais Mnangwagwa (75) ambae kitaaluma ni mwanasheria anafanya ziara hiyo huku akijiandaa na uchaguzi mkuu wa Rais na Wabunge utakaofanyika nchini Zimbabwe tarehe 30/Julai/2018,ikiwa ni kipindi cha mwezi mmoja kuanzia sasa. 


Uchaguzi huo unaelezwa kuwa utakuwa na mchuano na upinzani mkali hasa kufuatia mgombea wa chama kikuu cha upinzani ndugu Nelson Chamisa (40) kuelezwa kuwa anaungwa mkono na vijana wengi nchini humo. 


Ziara hii pia inakuja siku chache baada ya Rais Emmerson Mnangwagwa kunusurika katika shambulizi la bomu alipokuwa akihutubia wananchi katika kampeni za uchaguzi kwenye uwanja wa mpira wa miguu wa White City jijini Bulawayo tarehe 23/Juni/2018.


Kufuatia shambulizi hilo Rais Mnangwagwa alinukuliwa na BBC akituhumu kuwa shambulizi hilo lilikuwa ni la kupangwa na kundi la Generation 40 (Kikazi cha watu 40) G40 linaloongozwa na mke wa Rais Mstaafu wa nchi hiyo Robert Mugabe, Bibi Grace Mugabe. 


Katika mahojiano hayo na BBC Rais Mnangwagwa alisema:


"Sijui kama ilikuwa ni mtu mmoja; Ninafikiri ni jambo pana kuliko suala la mtu mmoja. Ninadhani huu ni mpango wa kisiasa kutoka kwa watu wenye chuki".


Rais Mnangwagwa amenusurika katika mashambulizi kadhaa ya kujaribu kumuua kwa miaka tofauti,kwani mwezi August mwaka 2017 Rais Mnangwagwa alinusurika kuuawa miezi mitatu kabla hajaondolewa kwenye nafasi ya Umakamu wa Rais lakini pia kabla ya hapo mwaka 2014 Rais Emmerson Mnangwagwa alinusurika kufa kwa kuwekewa sumu kwenye chakula ikiwa ni siku chache kabla hajateuliwa kuwa Makamu wa Rais. 


Ikumbukwe kuwa kundi la G40 liliwahi kumtuhumu Rais Mnangwagwa kwa kupanga mipango ya kutumia jeshi kumuondoa madarakani aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Robert Mugabe.


Tangu aingie madarakani,  Rais Mnangwagwa ameshafanya ziara kama hii katika nchi za Namibia, Zambia, Msumbiji,  Angola, Afrika ya Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Botswana. 


Kabla ya kuwa Rais wa Zimbabwe historia inaonesha kuwa Rais Mnangwagwa aliyezaliwa tarehe 15/Septemba/1942 alikuwa Makamu wa Rais wa nchi hiyo kuanzia mwaka 2014 na baadae kuondolewa kwenye nafasi hiyo tarehe 05/Novemba/2017 na aliyekuwa Rais wa nchi hiyo wakati huo Robert Mugabe kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kumdhania kuwa alikuwa akipanga njama za kumng'oa Rais Mugabe madarakani hali iliyopelekea Rais Mnangwagwa kukimbilia uhamishoni nchini Afrika ya Kusini. 


Rais Mnangwagwa alikuwa mtu muhimu na wa karibu kwa mtangulizi wake Rais Mstaafu Robert Mugabe wakati wa mapambano ya harakati za kupigania uhuru wa nchi hiyo dhidi ya wazungu wachache wakati huo Zimbabwe ikiitwa Rhodesia. 


Baada ya kuanzishwa kwa chama cha ZANU-PF mwaka 1963, Rais Emmerson Mnangwagwa alipatiwa mafunzo mbalimbali ya kijeshi katika nchi za China na Misti na baadae alirejea nchini mwake na kuunda kundi la harakati la vijana  lililojulikana kama *"Crocodile Gang"* (Mamba Wahuni) nae akipachikwa jina la *"Ngwena"* kwa lugha ya kabila lake la Washona likiwa na maana hiyo hiyo ya *"Mamba"* kwa lugha yetu ya Kiswahili. 


Mwaka 1965, Rais Mnangwagwa alikamatwa na kufunguliwa mashitaka ya "Ugaidi" na baadae kuhukumiwa adhabu ya kifo lakini wanasheria wake waliweza kumuepusha na adhabu hiyo kwa kutoa ushahidi uliothibitisha kuwa umri wake ulikuwa chini ya miaka 21 na hivyo kuhukumiwa kifungo cha miaka 10 jela ambapo alikutana na Rais Mstaafu Robert Mugabe na wakiwa huko gerezani wawili hao walianzisha harakati za pamoja kisiasa kupigania uhuru wa nchi hiyo juhudi ambazo baadae zilizaa matunda kwa Zimbabwe kupata uhuru. 


Baada ya Zimbabwe kupata uhuru mwaka 1980 Rais Mstaafu Robert Mugabe alikuwa Mwenyekiti wa ZANU-PF na Waziri Mkuu wa nchi hiyo huku Rais Mnangwagwa akiwa Waziri wa usalama wa taifa na Katibu Mkuu wa kwanza wa ZANU-PF. 


Rais Emmerson Mnangwagwa alihudumu katika nafasi nyingine mbalimbali katika nchi hiyo wakati wa utawala wa mtangulizi wake Rais Mstaafu Robert Mugabe kama Msaidizi maalumu wa Rais na mkuu wa kitengo cha raia na jeshi cha ZANU-PF mwaka 1977.


Waziri wa usalama wa taifa mwaka 1980 mpaka 1988


Mbunge Jimbo la Kwekwe Mashariki kuanzia mwaka 1985 mpaka mwaka 2000.


Katika mwaka 1988 mpaka mwaka 2000 kipindi hicho akiwa Waziri wa Haki, Sheria, na Mambo ya Bunge alipata kuhudumu pia kama Waziri wa fedha kwa siku 15 kufuatia waziri husika kupata changamoto. 


Kati ya mwaka 2000 na mwaka 2005 Rais Mnangwagwa alihudumu kama Spika wa Bunge la Zimbabwe.


Mwaka 2005 mpaka mwaka 2009 alihudumu kama Waziri wa Makazi ya vijijini na ustawi.


Mwaka 2008 Rais Mnangwagwa alipata kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Chirumanzu-Zibagwe


Kuanzia mwaka 2009 mpaka mwaka 2013 Rais Mnangwagwa alihudumu kama Waziri wa Ulinzi na baadae baada ya uchaguzi mkuu alirejea kuhudumu kama Waziri wa Haki, Sheria na Binge mpaka mwaka 2014 alipoteuliwa kuwa Makamu wa Rais.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini cha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirkiano wa Afrika Mashariki imeeleza kuwa  ziara ya Rais Emmerson Mnangwagwa ina malengo kadhaa moja likiwemo kujitambulisha kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli  na kwa wananchi wa Tanzania.


Sambamba na hilo ziara hii pia itatoa fursa ya kuimarisha na kukuza mahusiano mazuri yaliyopo ya kidiplomasia, kihistoria, kiuchumi na kijamii baina ya Tanzania na Zimbabwe.


Taarifa hiyo imeeleza kuwa viongozi hao watajadili masuala mbalimbali yanayohusu nchi hizi mbili kikanda kwa maana ya eneo kuwemo katika ukanda wa nchi za SADC na kimataifa kwa mazungumzo rasmi. 


Ikumbukwe vema kuwa Tanzania na Zimbabwe zilishiriki kikamilifu sambamba na nchi za Namibia, Angola, Msumbiji na Afrika ya Kusini katika kuliondoa na kuliangamiza kundi la waasi la M23 katika jimbo la Kivu kwenye nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC)  kati ya mwaka 2013 mpaka 2014.


Tunakumbuka vema aliyekuwa Mnadhimu Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya wananchi wa Tanzania (JWTZ) Luteni Jenerali Mstaafu James Aloizo Mwakibolwa wakati ule akiwa Brigedia Jenerali aliongoza vema mapambano ya kamandi ya vikosi alivyoviongoza vya kuleta amani nchini DRC (MONUSCO) kwa kingereza *Force Intervention Brigade (F.I.B).*


MONUSCO F.I.B ilikuwa imapewa mamlaka ya kuzima uasi wa M23 na Umoja wa Mataifa chini ya mpango wake wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC Resolution) namba 2098 la tarehe 28/Machi/2013.


Rais Emmerson Mnangwagwa anatarajiwa pia kutembelea Chuo cha Sanaa cha Kaole, Bagamoyo ambacho awali kilitumika kutoa mafunzo kwa wapigania uhuru kutoka nchi za Kusini mwa Bara la Afrika na Mheshimiwa Rais Mnangwagwa ni miongoni mwa waliopata mafunzo katika chuo hicho. 


Mheshimiwa Rais Mnangwagwa anatarajiwa kuondoka nchini tarehe 29/Juni/2018 kurejea nchini Zimbabwe na kuagwa na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt.John Pombe Magufuli.


Kwa ufupi ziara hii ya kikazi ya Rais Emmerson Dambudzo Mnangwagwa  nchini Tanzania inatoa taswira mbili kubwa kimataifa:


*(1) Tanzania bado inabaki kuwa sehemu muhimu ya darasa la siasa za kidola na harakati za ukombozi kwa nchi za Kusini mwa Bara la Afrika ikiwa ni alama ya harakati za uhuru wa bara zima la Afrika.*


*(2) Tanzania ni miongoni mwa mihimili mikuu kwa ulinzi, usalama,  amani duniani na ustawi wa bara bara la Afrika na hasa nchi zilizo Mashariki,  Kati na Kusini mwa Bara hili la Afrika.*


Kuthibitisha hilo hata Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Antonio Guterrez aliwahi kusimama kwa muda Tanzania akitokea Somalia na Kenya Jumatano ya tarehe 08/Machi/2017 ambapo alipokelewa na Wapiti wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Augustine Mahiga na Katibu Mkuu huyo wa UN kuelezea umuhimu wa Tanzania katika ulinzi wa amani katika eneo la pembe ya Afrika. 


Karibu Tanzania Rais Emmerson Dambudzo Mnangwagwa, Rais wa awamu ya Tatu wa Zimbabwe.


*Abbas Mwalimu.*


*+255 719 258 484*


*Uwanja wa Diplomasia.*
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top